UN yakubali kuharibu silaha za kemikali Syria

Image caption Wanachama wa baraza la usalama la UN wakipigia kura azimio hilo

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa pamoja bila pingamizi azimio la kutaka silaha za kemikali za Syria kuharibiwa.

Katika kikao cha baraza hilo mjini New York, baraza hilo lenye wanachama 15 liliunga mkono azimio hilo lililoafikiwa mapema mwezi huu kati ya Marekani na Urusi.

Azimio lenyewe linamaliza mzozo wa miaka miwili na nusu katika Umoja wa Mataifa kuhusu Syria , ambako mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi yangalil yanaendelea.

Kura hiyo imekuja baada ya wachunguzi wa kimataifa kuhusu silaha za kemikali, kukubaliana kuhusu mpango wa kuharibu silaha za Syria ifikapo katikati mwa mwaka 2014.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry amesifu diplomasia akisema kuwa ina nguvu sana kiasi cha hata kuharibu zana nzito za kivita. Aliipongeza jamii ya kimataifa kwa kusema kuwa imeweza kuafikia jambo muhimu sana.

Aidha aliitaka serikali ya Syria kutekeleza azimio hilo bila kuchelewa na pia kutangaza kuwa mkutano mwengine utafanyika mjini Geneva mwezi Novemba.

Ni wiki chache tu zilizopita, ambapo azimio hili lilionekana kutopigiwa kura katika baraza hilo kwani wanachama wa baraza hilo walikuwa wanazozana kwa miaka miwili unusu kuhusu Syria.

Lakini baada ya shambulizi la kemikali lililofanyika Agosti 21, wanachama wake hata hawangeweza kukubaliana kuhusu taarifa inayolaani vikali shambulizi hilo.

Azimio hilo linapendekeza kuwa Syria ikubali kuharibu silaha hizo ifikapo mwaka 2014 na wataalamu wa silaha kupewa fursa kuingia nchini humo kuhakikisha kuwa silaha hizo zote zimeharibiwa.

Lakini azimio lenyewe halitoi idhini ya moja kwa moja kuweza kuvamia Syria kijeshi ikiwa itakataa kutekeleza matakwa ya azimio hilo, kama alivyosisitiza waziri wa mambo ya nje wa Syria Sergei Lavrov.