Wasomali watafuta afueni Kismayo

Image caption Wengi wa wakimbizi wanaokimbilia Kismayo

Maelfu ya wasomali waliopoteza makao yao kutokana na vita, wanatoroka maeneo yanayodhibitiwa na wanamgambo wa Al Shabaab na kuishi katika kambi za wakimbizi katika mji wa bandarini wa Kismayo.

Vikosi vya kulinda amani vya Muungano wa Afrika, vinapambana na wanamgambo wa Al Shabaab katika mji huo.

Wengi wa waliopoteza makao yao, wanasema kuwa walihama kutoka makwao kwa sababu ya shinikizo za mara kwa mara na kuhangaishwa na wanamgambo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Mohamed Moalimu aliyezuru eneo hilo, wengi walioachwa bila makao ni akina mama na watoto wao.

Na sasa wanaishi katika makao ya muda kwenye kambi za wakimbizi mjini Kismayo, ambayo ni kambi rasmi ya vikosi vya AU.

Wengi walitoroka makwao na kuacha mali zao, kwa sababu walishindwa kuishi chini ya utawala wa sharia kali za Al Shabaab.

Waliongeza kusema kuwa kundi hilo linasajili watoto wao kuwapigania na wengi wao wamefunzwa itikadi za kundi hilo baada ya kuwapa silaha na mafunzo.

Mmoja wa wakimbizi hao ni Ali Hassan, babu ambaye anasema maisha katika kambi ni salama ikilinganishwa na walikokuwa wanaishi ingawa maisha ni ngumu kwa kuwa wamelazimika kuacha nyuma mali zao zote.

‘’Maisha yetu ni magumu, hatuna maji wala chakula hata dawa na kibaya mno ni kuwa watoto wetu hawana elimu,’’ alisema mzee Ali.

Naye mkimbizi mwengine, Yusuf Said ni baba wa watoto watano na anasema kuwa tatizo walilokuwa nalo ni wanamgambo wa Al-Shabaab ambao daima wamekuwa wakiwahangaisha.

Anasema waliwalazimisha kuwapa mbegu zao walizokuwa wanataka kupanda na kuwataka wawalipe kodi la sivyo wanyongwe.

Vikosi vya Amisom vimeitaka jamii ya kimataifa, kuwasaidia kukabiliana na idadi inayoongozeka ya wakimbizi wa ndani.

Brigedia Antony Ngere, ambaye ni komanda wa AMISOM Kusini mwa Somalia, alisema kuwa licha ya mashirika ya misaada kuwafikia wakimbizi hao, hali bado ni mbaya sana.

Kundi la Al Shabaab lingali linadhibiti sehemu kubwa ya Kusini mwa Somalia ambako wanawasajili vijana wasio na kazi na kuendeleza vita. Kundi hilo hufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga ndani na nje ya nchi hiyo.