Gambia yajiondoa kutoka Jumuiya ya madola

Image caption Rais Yahya Jammeh anasema Jumuiya ya madola ni njama tu ya ukoloni mamboleo

Taifa la Gambia linasema kuwa linajiondoa kutoka jumuiya ya nchi za madola baada ya kuwa mwanachama kwa miaka 48.

Nchi hiyo iliyo Magharibi mwa Afrika, imesema kuwa jumuiya hiyo yenye wanachama 54 ikiwemo Uingereza na nchi ambazo zilikuwa chini ya ukoloni wa Uingereza ni, ‘Taasisi ya ukoloni mambo leo.’

Hatua ya taifa hilo kujiondoa ilitangazwa kupitia kwa runinga ya taifa lakini hakuna sababu zengine zimetolewa.

Miaka miwili iliyopita, Rais Yahya Jammeh alikosoa Uingereza kwa kumuunga mkono mpinzani wake wa kisiasa, kabla ya uchaguzi mkuu.

Uingereza ilisema kuwa imesikitishwa sana na hatua ya Gambia kujiondoa kutoka Jumuiya ya Madola.

Mapema mwaka huu, Uingereza iliitaja Gambia kuwa moja ya nchi zisizoheshimu haki za binadamu, ikigusia jambo la watu kuzuiliwa kinyume na sheria, kufungwa kiharamu kwa magazeti na ubaguzi wa jamii zilizotengwa.

Mwezi Agosti mwaka jana Gambia ilikosolewa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu kwa kuwaua wafungwa tisa kwa kuwapiga risasi.

Jumuiya ya madola ilibuniwa mwaka 1931 lakini ikapata muundo wake wa kisasa baada ya mwaka 1949 wakati nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza kama vile Gambia, kuanza kujitawala .

Katika taarifa yake serikali ya Gambia imesema kuwa imejiondoa kama mwanachama wa Jumuiya hiyo na kuongeza kuwa haitawahi kuwa mwanachama wa taasisi ambayo inaendeleza ukoloni mamboleo.

Wakati wa mwisho taifa lolote lilijiondoa kutoka kwa Jumuiya ya Ulaya, ilikuwa mwaka 2003, wakati Zimbabwe ilipofuta uwanachama wake.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ye Uingereza, uamuzi wa nchi kujiondoa kutoka jumuiya yoyote ni jambo la nchi yenyewe kuamua. Lakini ni jambo la kusikitisha kwa Gambia kujiondoa kwa jumuiya hiyo, ilisema wizara hiyo.

Jumuiya hiyo ikiongozwa na Malkia Elizabeth wa pili mwenye umri wa miaka 87, itaandaa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama mwezi ujao nchini Sri Lanka