Jaji mkuu akamatwa kwa rushwa Indonesia

Image caption Maafisa wa kupambana na rushwa walimkamata Mochtar nyumbani kwake Jakarta

Jaji mkuu wa mahakama ya kikatiba nchini Indonesia amekamatwa kwa madai ya rushwa.

Akil Mochtar alikamatwa na maafisa wa kupambana na rushwa kwa madai ya kupokea dola laki mbili na nusu kama rushwa.

Kwa mujibu wa maafisa hao, kukamatwa kwa Mochtar ni tukio la kwanza la hivi karibuni kukamatwa kwa afisaa mkuu wa umma kuhusiana na rushwa aliyopokea akisikiliza kesi kuhusu uchaguzi.

Mahakama ya kikatiba ya Indonesia husikiliza kesi zote kuhusiana na uchaguzi.

Bwana Mochtar alichaguliwa mwaka huu kwa muhula wa miaka mitano kwa wadhifa huo katika mahakama ya kikatiba.

Alikamatwa kwake nyumbani mjini Jakarta baada ya mfanyabiashara ambaye pia ni mbunge kumkabidhi pesa, kwa mujibu wa msemaji wa tume ya kupambana na rushwa nchini humo.

Kesi hiyo ilihusishwa na utata ulioibuka katika uchaguzi uliofanyika kisiwani Borneo.

Watu wengine wawili wamekamatwa baada ya kuhusishwa na kesi hiyo.

Mwezi jana mahakama ya kupambana na rushwa ilimpata na hatia generali wa polisi Djoko Susilo kwa kosa la kutengeza pesa haramu.

Susilo alihukumiwa jela kifungo cha miaka 10 na kutozwa faini.