Uchunguzi wa DNA kwa viungo vya miili Kenya

Image caption Chumba cha kuhifadhia maiti cha baraza la jiji la Nairobi

Jamaa ya baadhi ya wakenya waliopotea kufuatia shambulizi la kigaidi la Westgate wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa chembechembe za DNA.

Polisi walitoa ombi hilo baada ya kupata viungo vya mwili katika jengo hilo.

Shambulizi la kigaidi lililodumu siku nne, lilifanywa na kundi la kigaidi la AL Shabaab na kuwaua watu 67 wakati wengine zaidi ya 39 hawajapatikana mpaka leo.

Mwandishi wa BBC Robert Kiptoo anasema kuwa kumekuwa na taarifa tatanishi kuhusu ikiwa miili yote imetolewa katika jengo la Westgate.

Angalau miili mitatu zaidi ilifikishwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City.

Al-Shabab, ni kundi la kigaidi la Kisomali, na wanamgambo wake walivamia jengo la Westgate kwa siku nne kuanzia tarehe 21 Septemba kulipiza kisasi wanachosema ni hatua ya Kenya kujihusisha na vita nchini Somalia.

Angalau familia nne zilikuja katika chumba hicho cha kuhifadhia maiti Jumatano asubuhi kutafuta wapendwa wao. Watatu kati yao walikuwa jamaa za wanajeshi waliofariki katika shambulizi hilo.

Mwili mmoja uliweza kutambuliwa na jamaa kabla ya hata kufanya uchunguzi wa DNA.

Maafisa sita wa usalama waliuawa katika shambulizi hilo wakati shughuli za kuwaokoa mateka zilipoanza.

Wanamgambo watano pia waliuwa na vikosi vya usalama lakini miili yao haijulikani iliko.

Watu tisa wangali wanazuiliwa baada ya kukamatwa kuhusiana na mashambulizi hayo.

Takriban wanajeshi 4,000 walikwenda Somalia, tangu mwezi Oktoba mwaka 2011 kusaidia wanajeshi wa serikali ya Somalia kumaliza vita vya miongo miwili na wanamgambo wanaopigania utawala wa nchi.