50 wauawa kwenye maandamano Misri

Image caption Vurugu mjini Cairo

Takriban watu 50 wameuawa kwenye makabiliano kati ya polisi na wafasi wa Rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi.

Zaidi ya wanachama wengine miambili wa vuguvugu la Muslim Brotherhood walikamatwa mjini Cairo,ambako vifo vingi zaidi viliripotiwa.

Wafuasi wa Morsi waliandamana katika miji kadhaa kote nchini Misri, huku jeshi likiadhimisha miaka 40 ya vita vya mwaka 1973 katika ya waarabu na waisraeli.

Wafuasi wa Morsi wanasema kuwa aliondolewa mamlakani na jeshi mwezi Julai mwaka huu.

Kipindi muhimu

Mamia ya watu walikusanyika katika medani ya Tahrir kuadhimisha siku hiyo.

Ndege za kijeshi zilionekana zikipaa angani huku jeshi likionyesha uwezo wake wa kulinda nchi.

Baadhi ya waliokuwa wamekusanyika mjini humo walishangilia wakiwa wamebeba mabango yenye picha za mkuu wa ulinzi Generali Abdel Fattah al-Sisi. Baadhi wanamtaka agombee urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Lakini mwandishi wa BBC Quentin Sommerville mjini Cairo anasema kuwa wafuasi wa Morsi pia waliandamana kwa wingi wakijaribu kuingia Tahrir kwa lazima huku wakimuita Generali Sisi muuaji.

Askari wa usalama walitumia moshi wa kutoza machozi na kufyatua risasi hewani kuwazuwia wafuasi wa Morsi kufika medani ya Tahrir mjini Cairo.

Maelfu ya watu walishiriki Tahrir katika shughuli zilizotayarishwa na jeshi kuadhimisha siku hiyo.

Ghasia piya zilizotokea katika maandamano kama hayo kwenye miji kadha mengine ya Misri.