Rwanda yakana madai ya watoto wanajeshi

Image caption Waasi wa M23

Serikali ya Rwanda imepinga vikali madai dhidi yake kuwa inasaidia kutoa mafunzo ya kijeshi kwa watoto wanaokwenda kupigania waasi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akiongea na BBC, waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo ametaja madai hayo kuwa ya kipuuzi sana.

Marekani imesitisha msaada wake wa kijeshi kwa Rwanda ikisema kuwa nchi hiyo inaunga mkono waasi wa M23 wanaoaminika kuwasajili watoto kuwapigania.

Waasi wa M23 wamewalazimisha maelfu ya watu kutoroka makwao Mashariki mwa DRC.

"dhana kuwa Rwanda ina uhusiano na watoto wanajeshi ni dhana potovu sana,'' Bi Mushikiwabo aliambia BBC.

"tumeshirikina na mashirika kadhaa ya UN , kuhakikisha kuwa watoto hawasajiliwi kama wapiganaji.''

Marekani ilikuwa na uhusiano mkubwa wa kijeshi na Rwanda tangu chama tawala cha (RPF) kuingia mamlakani baada ya mauaji ya kimbari kufanyika nchini humo mwaka 1994.

Rwanda imetuhumiwa kwa kuunga mkono waasi wa M23, ambalo linaongozwa na watu wa kabila laTutsi.

Aidha Rwanda imeshambulia DRC mara mbili ikisema kuwa inataka kuwakomesha wapiganaji wa Kihutu kuvamia mipaka yake.

Rais Kagame, mwenyewe ni wa kabila la Tutsi, na aliongoza chama cha RPF kilipomaliza mauaji ya kimbari ambapo watu 800,000 wengi wa Tutsi na wa Hutu wachache walifariki.