Libya yamhoji balozi wa Marekani kuhusu Liby

Image caption Majeshi ya Marekani yaliyomkamata Al Liby mjini Tripoli

Serikali ya Libya imemhoji balozi wa Marekani nchini humo kuhusu hatua ya majeshi ya Marekani kumkamata mshukiwa wa kundi la kigaidi la Al Qaeeda ndani ya nchi hiyo.

Anas al-Liby, alikuwa anasakwa kwa udi na uvumba tangu kuongoza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998.

Anas al-Liby alikamatwa Jumamosi na wanajeshi wa Marekani mjini Tripoli.

Waziri mkuu wa Libya, Ali Zeidan alisema kuwa uhusiano kati ya Marekani na nchi hiyo hautaathirika kutokana na kukamatwa kwa al Liby nchini humo.

Bwana Zeidan alisema kuwa raia wa Libya lazima wahukumiwe nchini Libya. Waziri wa haki na sheria naye akasema kuwa anahitaji maelezo kuhusu swala hilo.

Marekani imesema kuwa mpango wake wa kumkamata al Liby ulikuwa halali

Mwanawe Liby, Abdullah al-Ruqai, amesema kuwa babake alikamatwa na watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao na kuwa baadhi yao walikuwa raia wa Libya.

Anaamini kuwa serikali ya Libya pia ilihusika na kutoweka kwa babake, madai ambayo Libya imeyakanusha vikali.

Waziri wa sheria wa Libya Salah al-Marghani alitaka kikao na balozi wa Marekani kujadili swala hilo, Jumatatu asubuhi wakati maandamano yakifanyika mjini Benghazi kuhusu kukamatwa kwa Anas al-Liby.

Naye balozi wa Marekani aliambia BBC kuwa alikuwa katika mazungumzo na serikali ya Libya ikiwemo wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.

Bwana Marghani na maafisa wengine kutoka katika wizara ya mambo ya nje pia walikutana na familia ya Liby waliofahamishwa kuhusu mazungumzo yao na balozi wa Marekani.

Liby – ambaye jina lake la kweli ni Nazih Abdul-Hamed al-Ruqai – anaaminika kuwa mmoja wa wale walioongoza mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania na kusababisha vifo vya watu 220 .

Liby ameshitakiwa nchini Marekani kuhusiana na mashambulizi hayo na amekuwa kwenye orodha ya watu wanaosakwa sana na shirika la ujasusi la FBI kwa zaidi ya miaka kumi huku mwenye taarifa kumhusu akiahidiwa zawadi ya dola milioni 5.

Marekani imetetea hatua yake ya kumkamata al Liby ikisema kuwa walifanya hivyo kwa kuzingatia sheria na kuwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yake.