30 wauwa kwenye makabiliano CAR

Image caption Waasi wa Seleka wameingia jeshini

Takriban watu 30 wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa kwenye makabiliani katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Maafisa wanasema kuwa makabiliano yalizuka kati ya waliokuwa waasi na makundi ya kiraia ya ulinzi siku ya Jumatatu na kuendelea hadi Jumanne.

Duru zinaarifu kwamba makundi hayo ya kiraia ambayo hutoa ulinzi kwa raia, yalishambulia kijiji cha Garga kilicho umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu Bangui.

Nchi hiyo masikini, imetokomea kwenye ghasia tangu waasi waliokuwa wanaongozwa na rais Michel Djotodia kumwondoa mamlakani mtangulizi wake Francois Bozize mwezi Machi.

Raia katika kijiji cha Garga, walithibitisha kuwa mapigano yalizuka na kusababisha hadi vifo 60 huku baadhi ya taarifa zikisema kuwa wenyeji wa kijiji hicho walimalizwa.

Mwanzo taarifa zilisema kuwa wenyeji walishambuliwa na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa rais aliyeondolewa mamlakani.

Waasi kutoka kundi la Seleka lililomwondoa mamlakani aliyekuwa Rais Bozize waliingia kijijini humo na kuanza kuwatafuta waasi hao . Raia mmoja alisema aliona miili ya watu 40 na hakuna hata afisaa mmoja wa Seleka alikuwa miongoni mwa waliofariki.

Waasi wa Seleka waliohusika kwenye mapigano hayo walijumuisha wapiganaji kutoka nchi jirani ya Sudan , kwa mujibu wa taaifa za wenyeji.

Hata hivyo rais mpya aliwasihi wapiganaji wengi kusalimisha silaha na kuingia jeshini lakini waasi wa Seleka wamekuwa wakiendelea kufanya mashambulizi na kusababisha vijana kuanza kutoa ulinzi kwa raia.

Waasi hao ambao hawana mafunzo ya kijeshi wamekuwa wakidaiwa kupora kutoka katika vituo vya afya na kuwaibia raia mali zao tangu Rais Djotodia kuingia mamlakani.

Rais huyo ameahidi kuondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2016.