Uwanja Kenya uliteketea kutokana na hitilafu

Image caption Mamia ya watu walikwama kutokana na uwanja huo kuteketea

Moto ulioteketeza uwanja rasmi wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, ulitokana na hitilafu ya kimitambo wala sio shambulio la kigaidi.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa wachunguzi wa Marekani.

Kenya iliiomba Marekani kutumia shirika lake la ujasusi kuisadia kwa uchunguzi ili kuondoa wasiwasi kuwa uwanja huo huenda ulishambuliwa na magaidi.

Moto huo uliteketeza sehemu kubwa ya kuwasilia wageni wa kimataifa ya uwanja wa ndege na kuwaacha abiria wengi wakiwa wamekwama.

Ulisababisha kufungwa kwa muda kwa uwanja huo.

Moto huo hata hivyo ulidhibitiwa baada ya masaa manne.

Uwanja huo ni kitovu cha usafiri katika kanda hii na huwahudumia zaidi ya abiria 16,000 kila siku.

Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec, alishauriana na Rais Kenyatta kuhusu matokeo ya uchunguzi wa majasusi wa FBI, katika mkutano uliofanyika mjini Nairobi.

"Kenya itashauriana na washirika wake wa kimataifa, kuhusu maswala yote ya usalama, ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa salama, eneo zima na dunia nzima kwa ujumla,’’ alisema Rais Kenyatta.

Pia walijadili shambulizi la kigaidi liliofanywa na kundi la al-Shabab dhidi ya jengo la Westgate mjini Nairobi.

Takriban watu 67 waliuawa wakati wanamgambo wa Al Shabaab waliposhambulia jengo hilo kwa siku nne.