Ziara ya Rais Hollande Afrika Kusini

Image caption Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Hollande nchini Afrika Kusini

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, anaanza ziara yake ya Afrika Kusini hii leo kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuboresha ushirikiano na mataifa ya Afrika kuhusu mizozo.

Anatarajiwa kutia saini mkataba na mwenyeji wake Rais Jacob Zuma, kuhusu kuimarisha sekta ya kawi ya Nuklia nchini humo.

Ufaransa ni mshirika mkubwa wa kiuchumi wa Afrika Kusini na imekuwa kwa muda mrefu ikitaka kuimarisha uhusiano wa kisiasa kama sehemu ya juhudi za kubuni sera kuhusu Afrika.

Lakini nchi hizo mbili zimekuwa zikitofautiana kisiasa hasa hivi maajuzi tu kuhusu namna ya kushughulikia mzozo unaokumba Jumuhuri ya Afrika ya Kati na kabla ya kumwondoa mamlakani aliyekuwa rais wa Libya Kanali Muamar Gaddafi.

Lakini washauri wa Hollande wanasema kuwa ameendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Zuma kuhusu hali katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati ambako majeshi ya Ufaransa yalikwenda kupambana na waasi waliokuwa wanatatiza serikali baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa aliyekuwa Rais Francois Bozize mamlakani.

Wanajeshi 5 wa Afrika Kusini waliuawa na waasi hao wa Seleka na hivyo kulazimisha Afrika Kusini kuondoa majeshi yake nchini humo.

Ziara ya Hollande ni ya kwanza tangu Nicolas Sarcozy kuzuru taifa hilo mwaka 2008 kama sehemu ya kutaka kukuza uhusiano mpya na nchi hiyo.

Ufaransa ambayo ina ushawishi mkubwa barani Afrika,inajaribu sana kuiweka Afrika Kusini katika nafasi nzuri ya kuwa na jukumu kubwa kuhusu maswala ya usalama barani Afrika.