Ruto atoa vikwazo kwa mahakama ya ICC

Image caption Ruto amekanusha madai ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi Kenya mwaka 2007-2008

Naibu Rais wa Kenya , William Ruto, amesema kuwa ataacha kuitaka mahakama ya ICC kuakhirisha kesi yake kwa mwaka mmoja ikiwa majaji wataruhusu kesi dhidi yake kuendelea bila ya yeye kuwepo mahakamani.

Anataka aruhusiwe kurejea nyumbani kuendelea na majukumu yake wakati kesi yake ikiendelea.

Akiwahutubia waandishi wa habari mjini Hague ambako kesi yake inaendelea, Ruto alisema kuwa anataka kesi dhidi yake iendelee kwa sababu ana imani kuwa hana hatia ya kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007/2008.

Muungano wa Afrika ulipitisha azimio mnamo siku ya Jumamosi mjini Addis Ababa, Ethiopia ambalo lilisema kuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ni mtuhumiwa mwenza wa Naibu Rais Ruto, hapaswi kuhudhuria kesi dhidi yake mjini Hague mwezi ujao.

Hata hivyo Ruto amesema licha ya msimamo wa AU, yeye yuko tayari kuendelea kushirikiana na ICC ingawa amepinga vikali tuhuma dhidi yake.

Katika kikao maalum cha Muungano wa Afrika ulikosoa sana mahakama ya ICC na kulalamika kuwa ilikuwa inawasaka tu viongozi wa Afrika na hadi sasa tangu kuanzishwa kwake imemhukumu mtu mmoja tu ambaye alikuwa kiongozi wa waasi DRC Thomas Lubanga.

Muungano huo uliitaka mahakama kuakhirisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta chini ya kifungu cha kumi na sita cha mkataba wa Roma ambacho kinaruhusu kuakhirishwa kwa kesi hizo kwa mwaka au kutafuta njia nyengine ya kuziakhirisha.