Msajili wa Al Shabaab mahakamani Kenya

Image caption Kundi la Al Shabaab Somalia

Mwanamume anayeshukiwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab amefikishwa mahakamani nchini Kenya kwa tuhuma za kuwasajili vijana wa Kenya kujiunga na kundi hilo nchini Somalia.

Mwanamume huyo kwa jina Aden Mohamed Maalim mwenye umri wa miaka 38 kutoka nchini Somalia, alifikishwa mahakamani pamoja na vijana wawili wanaoshukiwa kuwa ndio walikuwa wamesajiliwa kujiunga na kundi hilo.

Inaarifiwa walikamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi mjini Garisa mwishoni mwa wiki wakiwa ndani ya basi iliyokuwa inatoka mjini Mombasa pwani ya Kenya, ingawa walikanusha madai ya kuwa na uhusiano na Al Shabaab.

Inaaminika kuwa walikuwa safarini kuelekea Somalia.

Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo aliamuru kuwa watatu hao waachiliwe kwa dhamana ya shilingi milioni mbili kila mmoja la sivyo wafungwe rumande hadi kesi yao itakaposikilizwa mwezi Februari mwaka ujao.

Juhudi za kupambana na ugaidi zimeshika kasi nchini Kenya hasa baada ya shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la kifahari la Westgate mjini Nairobi wiki tatu zilizopita kusababisha vifo vya zaidi ya watu sabini na kuwajeruhi mamia.

Kundi la kigaidi la Al Shabaab lilikiri kutekeleza shambulizi hilo na kusema kuwa lilikuwa linalipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha na vita nchini Somalia.

Jeshi la Kenya likishirikiana na wanajeshi wa Somalia pamoja na wengine kutoka Afrika wamekuwa wakipambana na Al Shabaab kiasi cha kuwafurusha kutoka mji mkuu Mogadishu na kutoka maeneo ya Kismayo ambako walikuwa wanajikimu kwa kutumia bandari.

Kundi hilo sasa hufanya mashambulizi ya kuvizia.

Sasa wanamgambo hao wako maeneo ya vijijini ambako wangali wanadhibiti pakubwa