Wito wa UN kwa DRC kuhusu mazungumzo

Image caption Waasi wa M23 wanaowahangaisha wananchi Mashariki mwa DRC

Mjumbe malum wa Umoja wa mataifa ametaka pande husika kurejelea mazungumzo ya amani kati ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na waasi wa M23.

Mjumbe maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu nchi za maziwa makuu mary Robinson amesema ni muhimu kwa pande zote kukamilisha mazungumzo hayo yaliyokuwa yakiendelea jijini Kampala, Uganda.

Mazungmzo hayo yalisitishwa kutokana na utata kuhusu suala la msamaha kwa waasi hao wa M23.

Baada ya mazungumzo ambayo Umoja wa Mataifa uliyataja kama ya kufana, utata uliibuka Jumatatu kuhusu kutolewa kwa msamaha kwa viongozi wa waasi wa M23.

Lakini sasa mjumbe huyo maalum, Mary Robinson ametaka pande zote kurejelea mazungumzo hayo na kuafikiana kuhusua masuala tata yaliyosalia kuhusu kujumuishwa kwa waasi hao wa M23 katika jeshi la serikali.

Bi Robinson amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba mazungumzo hayakukamilishwa.

Jumatatu, Robinson alifahamisha baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kutoka jijini Addis Ababa, kuhusu mwelekeo wa mazungumzo hayo.

Katika taarifa, Umoja wa Mataifa ulisema pande zote zilikuwa zimekubaliana kuhusu kuwachiliwa huru kwa wafungwa na kuvunjiliwa mbali kwa M23, kukiwa na pendekezo la kukifanya chama cha kisiasa.

Hata hivyo Robinson ameshutumu mashambulio ya hivi karibuni ya M23 kwa walinda usalama nchini humo.

Hayo yanajiri huku Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Dlamini Zuma, akizuru jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa kile afisi yake ilisema ni ziara ya kutathmini hatua zilizopigwa katika kuleta amani mashariki mwa Kongo.

Umoja wa mataifa kwa upande wake, umeshutumu Rwanda kwa kufadhili kundi hilo la M23, madai ambayo taifa hilo, limekanusha vikali.