AU yataka Kenyatta aachwe ushughulikie ugaidi

Image caption Muungano wa Afrika umekuwa ukilalamika kuwa ICC Inaionea sana Afrika

Muungano wa Afrika na Kenya zimelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuakhirisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto katika mahakama ya ICC, kwa mwaka mmoja ili waweze kukabiliana na tisho la ugaidi linalokumba taifa hilo.

Hii ni baada ya Kenya kushambuliwa na magaidi zaidi ya wiki tatu ziliopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 65 na mamia ya wengine kujeruhiwa.

Kundi la kigaidi la Al Shabaab lilikiri kushambulia jengo la maduka la Westgate kama hatua ya kulipiza kisasi hatua ya majeshi ya Kenya kuwa nchini Somalia kupambana na kundi la Al Shabaab.

Katika ujumbe wake kwa baraza la usalama la UN na ambayo shirika la habari la Reuters liliuona, viongozi wa Muungano huo wamesema kuwa kesi inayoendelea dhidi ya viongozi wa Kenya itawatatiza na kuwazuia kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

Viongozi wa Kenya wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia ghasi za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007-08.

ICC inadai kuwa waliongoza vita vya kikabila vilivyosababisha vifo vya watu 1,200 na kuwaacha maelfu bila makao.

Wote wamekanusha madai hayo na hata kuitaka mahakama kusitisha kesi hizo au kuziakhirisha.

Muungano wa Afrika hata hivyo uliwahi kuomba mahakama ya ICC kuhamisha kesi hizo ili kuwapa muda wa kuimiarisha vita dhidi ya na tisho la ugaidi na usalama katika kanda nzima.

Wajumbe wa baraza la usalama la UN hata hivyo,wamesema kuwa wanaweza wakatafakari ombi lolote la AU ingawa walikataa ombi la Kenya la kuakhirishwa kesi hizo mwaka 2011 na kukata ombi lengine mwezi Mei la kutaka kesi hizo kusitishwa likisema kuwa halina mamlaka ya kufanya hivyo.

Baraza la usalama hata hivyo linaweza kuidhinisha kuakhirishwa kwa kesi hizo chini ya kifungu 16 cha mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo miaka 10 iliyopita. Hata hivyo baraza hilo litahitajika kupitisha azimio la kulipa mamlaka ya kuahirisha kesi.