Malawi yaghadhabishwa na matamshi ya Zuma

Image caption Rais Joyce Banda

Serikali ya Malawi imeghadhabishwa na matamshi ya Rais wa Afrika Kusini Jacob Kusini yaliyoonekana kudharau miundo msingi nchini Malawi.

Malawi sasa imemtaka balozi mkuu wa Afrika Kusini nchini humo kuelezea matamshi ya kusikitisha yaliyotolewa na Rais Jacob Zuma kuhusu nchi hiyo.

Balozi huyo, Cassandra Makone alitakiwa na serikali ya Malawi kufafanua matamashi ya Zuma yaliyotafsiriwa na wengi kumaanisha kuwa Malawi bado iko nyuma sana alipokuwa anazungumzia miundo msingi ya Afrika Kusini.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Quent Kalichero aliambia shirika la habari la AFP kuwa Makone aliitwa na serikali ili kueleza alichomaanisha Rais Zuma.

Balozi huyo alifanya mkutano na afisaa mkuu katika wizara ya mambo ya nje George Mkondiwa ingawa Kalichero inaarifiwa alikataa kutoa maelezo ya mkutano.

Mnamo siku ya Jumatatu, Zuma alizua utata alipokuwa anawashawishi madereva wa nchi hiyo kukubali kutozwa kodi za barabarani mjini Johannesburg.

''Tuko mjini Johannesburg, na hii ni Johannesburg. Sio kama barabara ovyo ya kitaifa nchini Malawi,'' alinukuliwa akisema Zuma.

Hata hivyo msemaji wa Zuma Mac Maharaj alisema kuwa taarifa hiyo ilitafsiriwa visivyo.

Aliongeza kuwa Zuma alikuwa tu anasisitiza kuhusu mfumo mzuri wa barabara Afrika Kusini ikilinganishwa na nchi zengine katika kanda ya Afrika Kusini.

Hata hivyo, Maharaj aliomba radhi kwa matamshi hayo akisema kuwa watu wengi wameghadhabishwa nchini Malawi.