Serikali SA yabana matumizi kwa mawaziri

Image caption Serikali ya Afrika Kusini inataka kuokoa pesa zaidi ya dola milioni moja kwa mwaka

awaziri wa serikali ya Afrika Kusini hawataweza tena kusafiri katika darala la kwanza au sehemu ya First Class kwenye ndege wakati wa ziara zao nje ya nchi ,kusafiri ovyo kwa kutumia magari ya serikali pamoja na kutumia kadi za serikali za kukopa wakati wanapoishi katika nyumba za kupangisha.

Alipokuwa anawasilisha bajeti ya serikali bungeni, waziri wa fedha Pravin Gordhan alitangaza baadhi ya mipango ya kubana matumizi ya pesa za serikali ili kuzuia kuongezeka kwa deni la serikali.

Mipango ya kupunguzwa kwa matumizi ya pesa za serikali kwa maafisa wa serikali, ilitangazwa na waziri wa fedha

Pravin Gordhan ni mmoja wa mawaziri wa serikali waliojitwika jukumu la kutaka kuokoa zaidi ya randi bilioni 2 au dola milioni mioamoja za serikali.

Pamoja na mambo mengine Gordhan alitangaza kuwa serikali itatangaza bei jumla ya magari ya serikali.

Pia hawatakuwa tena na kadi za kukopesha bidhaa na kulipa baadaye , hawataishi tena katika hoteli za kifahari wakati wakifanya shughuli za serikali na mawaziri pia hawataboreshewa nyumba zao.

Pia watazuia maafisa wengi kuambatana na mawaziri wa serikali kwa safari za majukumu ya serikali kuanzia tarehe moja Disemba.

Gordhan aidha alisema kuwa serikali kamwe haitawapa mawaziri vileo katika hafla za serikali.

Hata hivyo, alipuuza suala la kuiboresha nyumba ya Rais Jacob Zuma itakayogharimu randi milioni ishirini, eneo la Nkandla lakini akasisitiza kuwa ikiwa ndege mpya ya rais itahitajika basi sharti inunuliwe.

Vyama vya upinzani vimepongeza hatua hiyo ya kupunguza matumizi ya pesa za serikali huku baadhi vikilalamika kuhusu muda wa tangazo hili vikisema kuwa tayari vitu hivyo vimegharimu serikali pesa nyingi sana.