Tunisia yawalilia maafisa waliouawa

Image caption Rais wa Tunisia Moncef Marzouki

Rais wa Tunisia ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia kuuawa kwa maafisa nane wa Polisi, kulikofanywa na watu wanaotuhumiwa kuwa wanamgambo katika jimbo la Sidi Bouzidi lililoko katikati mwa Tunisia.

Rais Moncef Marzouki amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka miwili ya uchaguzi huru wa kwanza nchini humo. Mapema waziri mkuu Ali Larayedh amethibitisha kuwa serikali itajiuzulu baada ya mazungumzo na wapinzani kuhusu uteuzi wa utawala wa mpito utakapokamilika. Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia uliodumu kwa miezi kadhaa.

Waziri mkuu amesema serikali yake inayoongozwa na chama cha Kiislam chenye msimamo wa wastani, kimedhamiria kuachia madaraka kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mpango huo wa amani.

"Hatusalimu amri kwa mtu yeyote isipokuwa kwa maslahi ya nchi," amesema.

Hotuba yake imetolewa baada ya maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali, kuandamana katika mji mkuu Tunis, wakitaka serikali ijiuzulu. Mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia umechochewa na kuuawa kwa wanasiasa wawili maarufu mapema mwaka huu. Hali hii inatishia kuharibika kwa mabadiliko ya kidemokrasia yaliyoanza baada ya wananchi wa Tunisia kuung'oa utawala wa kiimla mwanazoni mwa mwaka 2011, mabadiliko ambayo yamekuwa yakijulikana kama mageuzi ya nchi za Kiarabu. Mapema mwezi huu, chama tawala cha Ennahda kilikubali kuachia madaraka kwa kuunda serikali ya mpito ambayo itaendesha nchi hadi uchaguzi mpya utakapofanyika.

Chama cha Ennahda na upinzani wana wiki tatu za kuteua baraza la mawaziri la muda. Pia wana mwezi mmoja wa kupitisha katiba mpya, sheria za uchaguzi na kupanga tarehe ya kufanyika uchaguzi.