Watuhumiwa wa tukio la Tiananmen watajwa

Image caption Moto katika bustani ya Tiananmen,Beijing China

Polisi nchini China wamewataja watuhumiwa wawili wanaohusishwa na tukio la mjini Beijing, baada ya gari kugongeshwa kwenye bustani yaTiananmen na kusababisha vifo vya watu.

Gari hilo liliangukia katika umati watu katika bustani hiyo na kushika moto, ukiua watu watano.

Kufuatia tukio hilo la Jumatatu, polisi wametoa ilani kwa mahoteli mjini Beijing, wakitaka taarifa kuhusu watu wawili kutoka jimbo la Xinjiang, vyombo vya habari vya China vimesema.

Taarifa hiyo ya polisi pia imelielezea gari hilo, likiwa na vibao vinne vya namba za gari zilizosajiliwa kutoka Xinjiang.

"Tukio kubwa limefanyika Jumatatu, ilani ya polisi imesema," bila ya kubainisha. Taarifa hiyo imewataja raia wawili kutoka jimbo la Xinjiang kama watuhumiwa.

Taarifa hiyo, ambayo imesambazwa katika vyombo vya mawasiliano ya kijamii nchini China, pia imewataka wasimamizi wa mahoteli kuwabaini wageni wanaotiliwa mashaka pamoja na magari.

Xinjiang ni makaazi ya kundi la waislam wachache wa kabila la Uighur. Baadhi ya watu wa kabila la Uighur wamelalamikia kubaguliwa kiutamaduni na kidini na utawala wa Beijing, na kumekuwa kukizuka ghasia za hapa na pale mjini Xinjiang. China inasema watu wa Uighur wamepewa uhuru mkubwa.

Jumatatu, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, alisema hajui undani wa tukio hilo.

Bustani ya Tiananmen ni eneo nyeti kutokana na kuhusishwa kwake na maandamano ya mwaka 1989 yaliyolenga kutetea demokrasi, ambayo yalimalizika kwa msako wa kijeshi.

Kwa ujumla eneo hili liko katika ulinzi mkali kutokana na kuwa karibu na taasisi za kisiasa na kwamba lisitumike kuwa kitovu cha waandamanaji na wapinzani, licha ya matukio ya ghasia kutokea katika eneo hilo hapo kabla.