Israel yawaachilia wafungwa wa Palestina

Image caption Waisraeli wengi walipinga kuachiliwa kwa wafungwa wa Palestina

Serikali ya Israel imewaachilia wafungwa 26 wa Palestina kama sehemu ya makubaliano ya kuanza tena mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili.

Wafungwa watano, waliachiliwa katika Ukanda wa Gaza wakati wengine 21 wakipelekwa katika Ukingo wa Magharibi.

Wale walioachiliwa walikuwa wamehukumiwa kwa kosa la mauaji na walikuwa wameishi jela kwa kati ya miaka 19 na 28 .

Maafisa wa Israel na Palestina walianza tena mazungumzo mjini Jerusalem mnamo mwezi Agosti, baada ya miaka mitatu ya kutatizika kwa mazungumzo hayo ya amani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC katika Ukingo wa magharibi,Yolande Knell wale walioachiliwa wanaonekana kama wafungwa wa kisiasa na mashujaa wa harakati za ukombozi wa wapalestina , lakini uamuzi wa kuwaachilia wafungwa hao haujawafurahisha wengi nchini Israel.

Wapalestina walioachiliwa mapema Jumatano, walitolewa kutoka jela la Ofer na kupelekwa katika kivukio cha Erez kuingia Gaza na katika kivukio kingine cha Beituna kuingia Ukingi wa Magharibi.

Katika Ukanda wa Gaza watu walipiga baruti huku waliokuwa wafungwa hao wakiingia Palestina kwa msururu wa magari.

Kwenye Ukingo wa Magharibi, walipelekwa katika eneo la Ramallah ambako Rais wa Palestina alikuwa anahutubia umati mkubwa wa watu.

Abbas alisema kuwa wafungwa wengine wataachiliwa katika kipindi cha miezi miwili, na kutoa wito wa kuachiliwa huru kwa wapalestina wote waliofungwa.

"Hapatakuwa na makubaliano ya mwisho bila ya kuachiliwa kwa wafungwa wote wa Palestina,’’ alisema Rais Abbas.

Pia alikanusha tetesi kuwa makubaliano ya kauchiliwa kwa wafungwa yaliafikiwa baada ya Israel kuruhisiwa kujenga makaazi zaidi ya walowezi katika eneo hilo.

Hatua ya kuachiliwa kwa wafungwa imesababisha mgawanyiko katika muungano tawala nchini Israel, huku vyama vyenye msimamo mkali vikitaka kuzuia shughuli hiyo kuendelea.