Mateka 4 wa Ufaransa waachiliwa Niger

Image caption Serikali ya Ufaransa imekanusha madai kuwa imelipa kikombozi ili wanne hao kuachiliwa

Mateka wanne wa Ufaransa waliokuwa wamezuiliwa nchini Niger tangu mwaka 2010, wameachiliwa.

Tangazo hili limetolewa na Rais wa nchi hiyo Francois Hollande.

Alisema kuwa Mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wamekwenda nchini Niger na kuwa mateka hao watarejeshwa nyumbani haraka iwezekanavyo.

Waziri wa ulinzi alisema kuwa wanaume hao wanne waliachiliwa bila ya kuhusishwa kwa jeshi wala kulipwa kwa kikombozi.

Walikamatwa tarehe 16 mwezi Septemba mwaka 2010 katika uvamizi dhidi ya kampuni ya madini ya Uranium karibu na mji wa Arlit.

Kundi la kigaidi katika kanda hiyo lilikiri kuwateka nyara watu hao.

Marafiki na jamaa zao wamefurahi sana kwani hawakujua ni lini wanaume hao wangeachiliwa huru.

Familia za wanne hao bila shaka wameghadhabishwa kutokana na kupokea taarifa hiyo kupitia kwa vyombo vya habari kwani hawakupewa taarifa zozote na serikali, lakini sasa inaonekana kuwa kimya cha serikali kilikuwa na sababu kuu.

Wanne hao inaonekana kwamba waliachiliwa nchini Mali.

Kundi la wapiganaji wa kiisilamu la AQIM, lina kambi yake katika aneo la Kaskazini mwa Mali. Lakini maeneo hayo yalipovamiwa na jeshi la Ufaransa wakati wa operesheini yao dhidi ya makundi ya wapiganaji wa kiisilamu, wapiganaji hao walilazimika kutawanyika.

Serikali ya Ufaransa imekanusha vikali kulipa kikombozi ili kuachiliwa kwa wanne hao, lakini kampuni iliyokuwa imewaajiri wanne hao huenda ilifanya kila ililoweza kuhakikisha usalama wao.