Kiongozi wa waasi wa M23 ajisalimisha

Image caption Bertrand Bisiimwa kiongozi wa waasi wa M23

Kiongozi wa waasi wa M23 Bertrand Bisiimwa ameripotiwa kusalimu amri kwa jeshi la Uganda.

Kiongozi huyo wa waasi alivuka na kuingia nchini Uganda kwenye masururu wa magari mawili huku wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na wale wa DRC walipofika kilomita tano kuelekea katika kambi yake ya kijeshi

Mwandishi wa BBC Ignatius Bahizi amesema baada ya kuongea na afisaa mmoja wa usalama eneo la Bunagana alimthibitisha kujisalimisha kwa Bisiimwa akisema kuwa anahojiwa na maafisa wa usalama katika eneo la Bunagana katika mpaka wa Uganda na Congo DRC.

Waasi wa M23 mnamo siku ya Jumatatu walitoroka maeneo yao ya vita ikiwemo eneo la Rumangabo baada ya kukabiliwa na mashambulizi kutoka kwa jeshi la UN na sasa inaarifiwa wametorokea msituni.

Majeshi yanayopambana na waasi hao yamefanikiwa kuwashinda waasi hao katika miji waliyokuwa wameiteka na sasa kuna matumaini kuwa jeshi la DRC linaweza sasa kusitisha harakati za kundi hilo ambazo zilianza miezi 20 iliyopita na ambazo zimewasababisha maelfu ya watu kutoroka makwao wakikimbilia usalama wao.

Kundi hilo limekuwa kikiendeshea harakati zao katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa aliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa siku ya jumanne kuwa waasi wa M23 sio tisho tena na kuwa wameshindwa kijeshi baadhi wakikimbilia msituni kutokana na mashambulizi makali kutoka kwa wanajeshi wa muungano wanaokabiliana na waasi hao.

Naye msemaji wa UN nchini Uganda amesema kuwa zaidi ya watu 5,000 wametoroka maeneo ya Bunagana kufutaia mapambano makali kati ya waasi na wanajeshi wa DRC.

Lucy Beck wa shirika la kuwahudumia wakimbizi alisema Jumatano kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka hadi 10,000 ifikapo siku ya Alhamisi huku mapambano yakichacha katika mpaka wa Uganda na Congo.