US:Nia ya viongozi ndio sababu ya udukuzi

Image caption Mkrugenzi wa upelelezi nchini Marekani James Clapper

Mkuu wa ujasusi nchini Marekani, James Clapper amesema kuwa nia ya baadhi ya viongozi wa kimataifa ndio moja ya sababu kuu ya Marekani kufanya upelelezi.

Mkurugenzi wa shirika la kitaifa la upelelezi, James Clapper, katika kutetea sababu yao ya kuwapeleleza viongozi wa kimataifa , alisema kuwa juhudi kama hizo ni muhimu sana katika sera ya upelelezi ya Marekani.

Lakini aliambia kamati ya waakilishi wa bunge kuhusu upelelezi, kuwa Marekani haipelelezi mataifa ya kigeni kwa undani na kiholela.

Bwana Clapper alikuwa anajibu tuhuma dhidi ya Marekani kufuatia ripoti za udukuzi dhidi ya viongozi wa kimataifa na ambao ni washirika wakuu wa taifa hilo.

"Nia ya viongozi ndio moja ya sababu kuu ya kwa nini tunafanya upelelezi na kuutathmini,'' alisema Clapper akiongeza kuwa washirika wa kimataifa a Marekani pia huchunguza maafisa wa Marekani na mashirika mengine kama sehemu ya mipangilio ya serikali.

Alisema kuvuja kwa taarifa kuhusu shughuli za upelelezi wa Marekani dhidi ya mataifa mengine imeharibia nchi hiyo sifa yake na kuwa alitarajia taarifa zaidi kutolewa.

Rais Obama anasema kuwa anataka kubadili namna nchi hiyo inavyokusanya ujasusi wake.

Lakini alisema hakuna nchi nyengine iliyo na uwezo wa kukusanya upelelezi kama Marekani na kuwa kulikuwa na makosa yaliofanyika ambayo ni ya kibinadamu au yaliyotokana na hitilafu za kimitambo.

Mwandishi wa BBC Jonny Dymond mjini Washington alisema kuwa ikiwa mtu yeyote alikuwa anatarajia kuombwa radhi na Marekani basi ajue kuwa hilo haliwezi kufanyika.