Mugabe anaweza 'kutusiwa' au kukosolewa

Image caption Watu kadhaa wameshitakiwa nchini Zimbabwe kwa kumtusi Rais Robert Mugabe

Mahakama ya kikatiba nchini Zimbabwe imebatilisha sheria inayosema kuwa ni uhalifu kumtusi Rais wa nchi.

‘‘Viongozi wa mashitaka hawapaswi kuwa na tamaa sana ya kuwashitaki watu wanaomkosoa Rais Mugabe katika kumbi za ulevi na maeneo mengine ya kijamii,’’ iliamua mahakama ya kikatiba.

Angalau watu 80 wameshitakiwa chini ya sheria hiyo katika miaka ya hivi karibuni.

Mnamo mwezi Mei, mwanaharakati Solomon Madzore alikamatwa baada ya kudaiwa kumuita Mugabe 'Punda anayechechemaa.'

Alikanusha kosa la kumtusi Rais.

Chini ya kifungu cha 33 cha sheria ya uhalifu nchini Zimbabwe, mtu anaweza kufungwa jela hadi mwaka mmoja au kutozwa faini ya dola 100 kwa kumtusi Rais.

Sheria hiyo ilipingwa na watu kadha nchini humo akiwemo mkaazi mmoja wa mji wa Bulawayo Kusini mwa nchi, Tendai Danga, aliyekamatwa miaka miwili iliyopita kwa madai ya kumtusi Mugabe wakati alipozozana na polisi ndani ya baa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Harare, Brian Hungwe, majaji tisa waliotoa uamuzi huo, walikubaliana kwa kauli moja kuwa sheria hiyo inahujumu uhuru wa kujieleza na kuifanya vigumu kwa serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi wao.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilimpa waziri wa sheria, Emmerson Mnangagwa hadi tarehe 20 Novemba kukata rufaa.

Mwezi Agosti mahakama ilimwachilia huru mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 26 Takura Mufumisi, aliyeshitakiwa kwa kuwa na nia ya kutumia bango la karatasi lenye picha ya Mugabe kama karatasi ya kujipangusia chooni ndani ya baa moja.

Katika kura ya maamuzi iliyofanyika mwezi Machi, wananchi walipitisha katiba mpya ambayo inawapa uhuru zaidi wa kujieleza.

Watu wengi wamepongeza uamuzi wa mahakama wakiamini kuwa sheria ilikuwa imemlinda rais dhidi ya kukosolewa.