Jela maisha kwa ubakaji Afrika Kusini

Image caption Johannes alikiri kumbaka Anene lakini alikanusha madai ya kumuua

Mwanamume mmoja nchini Afrika Kusini aliyepatikana na hatia ya ubakaji na mauaji ya msichana mwenye umri wa miaka 17 amepewa hukumu mbili za maisha jela na mahakama moja viungani mwa mji wa Cape Town.

Viongozi wa mashitaka walitaka mshukiwa Johannes Kana afungwe jela maisha bila dhamana.

Marehemu Anene Booysen alifariki mwezi Februari , masaa kadhaa baada ya kuuawa kinyama katika kesi ambayo imewaghadhabisha wengi.

Afrika Kusini ni nchi mojawapo yenye visa vingi vya ukatili wa kijinsia duniani.

Mwandishi wa BBC Nomsa Maseko aliyefika katika mahakama ya Swellendam, umbali wa kilomita 220 kutoka mji wa Cape Town, anasema kuwa mjombake Kana alishanga kwa kupiga makofi na hata kuangua kicheko jaji alipotoa uamuzi wake.

" Hiki ni kichekesho ," alisema huku akiongeza kuwa mfumo wa sheria hauna haki

Lakini wengi waliohudhuria kesi hiyo walihisi kama haki imetendeka

Bi Booysen alitendewa ukatili na mwili wake kutupwa karibu na nyumba yake Bredasdorp lakini alifariki baadaye hospitalini mjini Cape Town

Wakati huohuo, Rais Jacob Zuma alitaja mauaji hayo kama ya kushtua na ya kinyama.

Ametoa wito kwa majaji kutoa adhabu kali sana kwa wanaofanya vitendo vya uhalifu wa kijinsia.

Wakati wa kesi dhidi ya Kana, madaktari waliomtibu Bi Booysen walisema kuwa majereha aliyoyapata yalikuwa mabaya zaidi kwake kuwahi kuyashuhudia.

Kabla ya kifo chake alisema kuwa karibu wanaume watano au sita walihusika na shambulizi dhidi yake , lakini washukiwa watatu walikamatwa baadae ingawa ni mmoja tu aliyehukumiwa.

Kana alikiri kosa la ubakaji ingawa alikana kuwa alimuua.