Marekani: Udukuzi ulivuka mipaka

Image caption Serikali ya Marekani inanuia kufanyia mageuzi mfumo wa upelelezi wa nchi hiyo

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema kuwa katika baadhi ya visa vya udukuzi vilivyofanywa na Marekani vilivuka mipaka.

Bwana Kerry kama afisaa mkuu zaidi katika serikali ya Rais Obama, ndiye wa kwanza kuzungumzia kashfa hii ambayo imewakera sana washirika wao wa Ulaya.

Alisema kuwa atashirikiana na Rais kuzuia vitendo kama hivyo vinavyofanywa na shirika la usalama wa kitaifa.

Kauli yake inakuja huku mataifa ya magharibi yakilalamikia madai kuwa Australia ilihusika katika kashfa ya upelelezi ya Marekani.

China imetaka maelezo kuhusu ripoti hizi za udukuzi huku Indonesia ikimtaka balozi wa Australia nchini humo kufafanua madai hayo.

Katika kauli yake , Kerry ametetea haja ya ongezeko la visa vya udukuzi akisema kuwa imeweza kuzuia visa vya ugaidi.

''Kwa sababu ya upelelezi tumeweza kuzuia ajali za ndege, majengo kulipuliwa na watu kutoshambuliwa kwa sababu tumeweza kujitahadhari kabla ya hatari,’’ Kerry aliambia kongamano moja mjini London.

Nawahakikishia kuwa watu wasio na hatia hawatafanyiwa upelelezi, lakini kuna juhudi za kujaribu kukusanya taarifa . Na ndio, katika visa kadhaa ambavyo vimeripotiwa, bila shaka vimevuka mipaka.

"Na Rais wetu , atajitahidi kuweka mambo wazi na kusema atafafanua na kuhakikishia watu kuwa anafanya kila kitu kuhakikisha kuwa atafanyia mageuzi mfumo mzima wa ujasusi na kuwa hakuna atakeyehisi kuwa amedhulumiwa na kwamba tutahakikisha jambo hili halitatokea tena ,’’ alisema Kerry.

Madai kuwa Marekani ilifanya upelelezi wake na kuwalenga viongozi wa nchi za kigeni imetatiza uhusiano wa kidiplomasia na washirika wake wa Ulaya.