Bangladesh yatoa hukumu ya kifo

Ukatili uliotokea wakati wa vita vya Pakistan mwaka '71 na kufanya Bangladesh kujitenga

Mahakama maalumu ya Bangladesh ya kusikiliza uhalifu wa vitani yametoa hukumu ya kifo kwa Wabangladeshi wawili walioko uhamishoni, kwa kushiriki kwenye mauaji ya wasomi na waandishi wa habari 18.

Mauaji hayo yamedaiwa kutokea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Pakistan mwaka wa 1971, ambavyo vilipelekea Bangladesh kujitenga na Pakistan.

Upande wa mashtaka uliiambia mahakama mjini Dhaka kwamba Chowdhury Mueen-Uddin - ambaye sasa anaishi Uingereza - na Ashrafuzzaman Khan - sasa raia wa Marekani - walikuwa katika kundi la wanamgambo ambalo likiunga mkono jeshi la Pakistan.

Wanaume hao wawili walifanyiwa kesi bila ya kuwepo na wamekanusha mashtaka hayo.

Serikali iliwapatia mawakili kuwatetea ingawa hakuna shahidi aliyeitwa kwa upande wao.