30 wauawa kwenye msafara wa harusi Nigeria

Image caption Licha ya serikali kutangaza hali ya hatari Mashariki mwa Nchi Boko Haram wangali wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara

Watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki nchini Nigeria, wameshambulia msafara wa harusi na kuwaua zaidi ya watu 30.

Shambulizi hilo lilitokea katika eneo ambalo hushuhudia visa vingi vya utovu wa usalama, kati ya miji ya Bama na Banki katika jimbo la Borno , Mashariki mwa mji mkuu wa jimbo hilo Maiduguri.

Bwana Harusi ni miongoni mwa waliouawa.

Kundi la wapiganaji wa Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara licha ya serikali kutangaza hali ya hatari Kaskazini Mashariki mwa Nigeria mwezi Mei.

Maelfu ya wanajeshi wa ziada, wametumwa katika eneo hilo kupambana dhidi ya Boko Haram, ambalo linapigana dhidi ya serikali tangu mwaka 2009 wakitaka kubuni utawala wa kiisilamu.

Hata hivyo, mashambulizi dhidi ya rais yameendelea.

Wiki moja iliyopita, mamia ya watu waliuawa wakati wa makabiliano kati ya wapiganaji hao na wanajeshi wa serikali, waliposhambulia mji wa Damaturu, kuchoma majengo ya polisi na jeshi.

Dereva mmoja aliyeona miili hiyo, aliambia shirika la habari la AFP kuwa wengi wa waathiriwa walikuwa na majeraha ya risasi.

Hali ya bibi harusi na familia yake haijulikani.