Morsi amwambia jaji 'angali Rais'

Kesi dhidi ya aliyekuwa rais wa Misri Mohammed Morsi imeahirishwa muda mfupi baada ya Morsi kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuchochea mauaji.

Morsi alimwambia jaji kuwa mashitaka dhidi yake sio halali kwani yeye angali rais wa Misri na ambaye alichaguliwa kwa njia ya demokrasia.

Baada ya matamshi ya Morsi, yalisababisha jaji kuahirisha kesi dhidi yake na kusema kuwa itasikilizwa tarehe nane mwezi Januari.

Wanachama wengine 14 wa ngazi za juu wa kundi la Muslim Brotherhood pia wameshitakiwa na mashitaka kama hayo.

Kesi hiyo inafanyika katika kituo cha mafunzo ya polisi ambapo kuna ulinzi mkali.

Vyombo vya habari vya kitaifa vimeripoti kwamba jaji wa kesi hiyo alilazimika kusitisha kwa mda kesi baada ya washtakiwa kuimba huku bwana Mosri akikataa kuvaa vazi la mahakamani akidai kuwa yeye nidye rais halali.

Mohammed Morsi alifikishwa katika chuo hicho kwa ndege aina ya helikopta kutoka eneo la siri ikiwa ndio mara yake ya kwanza kuwahi kuonekana hadharani tangu aondolewe mamlakani mwezi Julai mwaka huu.

Makundi ya waandamanaji tayari yamekusanyika nje ya chuo hicho cha mafunzo ya polisi huku wengine wakiimba nyimbo za kupinga jeshi la taifa hilo.

Maafisa wa kijeshi katika taifa hilo wanaendelea kushika doria katika mji wa Cairo na miji mingine baada ya wafuasi wa Bwana Morsi kuitisha maandamano makubwa.

Morsi aliondolewa uongozini kwa nguvu za jeshi mwezi Julai baada ya maandamano ya kila mara kufanyika kupinga utawala wake.

Ingawa alishinda urais kwa njia ya demokrasia, wakati wa uongozi wake wa zaidi ya mwaka mmoja, Morsi hakuelewana sana na taasisi nyingi za serikali.

Image caption Polisi na jeshi wamedhibiti hali ya usalama kote Misri

Baada ya kupinduliwa na jeshi, maandamano yalifanyika kila kulipokucha mjini Cairo na makubwa zaidi yalikuwa ya wafuasi wake kukesha karibu na kasri la rais wakitaka Morsi aachiliwe.

Polisi walaisababisha mamia ya vifo vya wafuasi hao walipovunja maandamano yao kwa nguvu.

Serikali ya muda pia imekuwa ikiwasawa na kuwakamata wanachama wa Muslim Brotherhood, chama chake Morsi.

Serikali pia imeharamisha vyama vyote vya kisiasa huku ikiwakamata mamia ya viongozi wa mashirika hayo.

Wafuasi wake wanasema kuwa alipinduliwa na jeshi na sasa anakabiliwa na kesi ya kisiasa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yameituhumu maafisa wa usalama kwa kufanya kazi yao bila uwajibikaji.