Mapigano yapamba moto DRC wengi wakitoroka

Image caption Wanajeshi wa DRC wakishangiliwa baada ya kukomboa mji wa Bunagana

Watu wote wa mji wa Bunagana Mashariki mwa DRC, wametoroka mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23.

Mwandishi wa BBC aliye katika eneo la mpaka wa Uganda na DRC, amesema kuwa makombora yaliyorushwa na wanajeshi yalisababisha vifo vya watu wanne.

Majeshi ya serikali siku ya Jumatatu yalikataa mazungumzo na waasi wa M23 waliokuwa wameahidi kusitisha vita kwa ajili ya kufanya mazungumzo na serikali ya DRC.

Karibia watu laki nane wametoroka makwao tangu mgogoro huu wa kisiasa kuanza Machi mwaka 2012.

Wiki jana , mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Martin Kobler, alisema kuwa kundi la M23 sio tisho tena kwa jeshi la DRC.

Siku moja baada ya kauli yake bwana Kobler, wanajeshi wa serikali waliukomboa mji wa Bunagana uliokuwa kombe kuu ya waasi hao, kwenye mpaka wa Uganda na DRC.

Hata hivyo, mapigano mapya yalizuka Jumatatu na hali ni tete sana mpakani mwa nchi hizo mbili huku wakaazi wakikimbilia usalama wao.

Wakimbizi wamefahamisha Bahizi kuwa ni wanajeshi wa serikali ya DRC waliosalia mjini Bunagana, huku maelfu ya wakaazi wakiwa wamekimbilia usalama wao na kuingia Uganda.

Aidha taarifa zaidi zinasema kuwa waasi hao nao wanaonekana kujibu mashambulizi dhidi yao kwa ukali mno ikilinganishwa na hali ilivyokuwa siku za awali.

Lakini wanajeshi sasa wameweza kukomboa mji muhimu wa Mbuzi ulio juu milimani karibu na mji wa Bunagana, baada ya kuushambulia kwa roketi na vifaru.

Waasi saba walikamatwa kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

"Ushindi, ushindi," wanajeshi waliokuwa katika mji jirani wa Ntamugenga walisikika wakisema, baada ya kupata habari kuwa mji wa Mbuzi umekombolewa.

Wanajeshi wa serikali sasa wanalenga maeneo matatu yaliyo milimani ambako waasi wengi wangali wamejificha.