Kongamano la amani Syria laahirishwa

Image caption Lakhdhar Brahimi anasema atahakikisha mkutano unafanyika angalu kabla ya mwisho wa mwaka

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika jumuiya ya nchi za kiarabu, amesema kuwa kongamano la amani kuhusu Syria lililokuwa limepangwa kufanyika mjini Geneva mwezi huu , limeahirishwa.

Mjumbe huyo Lakhdar Brahimi hata hivyo amesema kuwa angali ana matumani ya kufanyika kongamano la amani ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Amesema kuwa baada ya kukutana na wanadiplomasia wakuu, hakuwa tayari kutangaza tarehe ya mkutano huo.

Juhudi za kuandaa kongamano kati ya serikali na wapiganaji nchini Syria, zimekuwa zikiendelea kwa miezi kadhaa sasa baada ya kutokwepo maelewano kuhusu nani ahudhurie mkutano huo pamoja na ajenda ya mkutano wenyewe.

Bwana Brahimi amesema atakutana wanadiplomasia wa Marekani na Urusi kwa mara nyingine tarehe 25 , Novemba.

"Tulitumai kuwa tungeweza kutangaza tarehe ya mkutan huo leo, lakini ka bahati mbaya hilo halitafanyika,’’ Brahimi aliambia waandishi wa habari.

Mjumbe huyo aliongeza kusema kuwa hakuna kikubuwa kilichofanyika katika mazungumzo yaliyofanyika Jumanne na kwa kwamba sio ajabu tarehe ya mkutano haikuamuliwa.

Brahimi alikutana na mawaziri wa Marekani na Urusi na kisha baadaye kukutana na wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo Uingereza, Ufaransa, na China pamoja na chi jirani za Syria, Lebanon, Iraq, Jordan na Uturuki.