'Siachi siasa hadi nipate dola milioni 1'

Image caption Victoria Hammah amekuwa akisema amekuwa na shinikizo la kuiba pesa za umma

Naibu waziri wa mawasiliano nchini Ghana Victoria Hammah ameachishwa kazi baada ya kunukuliwa akisema kuwa atasalia katika siasa hadi atakapo pata fedha kiasi cha dola milioni moja.

Anaonekana katika kanda ya video akisema kuwa ukiwa na pesa unaweza kuwashawishi watu. Bi Hammah bado hajatoa tamko lolote kuhusiana na mkanda huo wa video au hatua ya kufutwa kazi.

Mwandishi wa BBC mjini Accra anasema Bi Hammah alikuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa rais John Mahama mwaka jana.

Baada ya uteuzi wake baadhi ya wadadisi walionya kuwa ana umri mdogo sana kuweza kuhudumu katika serikali.

Mwezi Agosti alinukuliwa akisema kuwa kuna shinikizo za kumtaka aibe fedha za umma kwa kuwa watu hudhani kwamba yeye ni tajiri kwa sababu ya wadhifa wake wa uwaziri.

Katika kanda hiyo alisikika akisema kuwa hatatoka katika siasa hadi atakapopata dola milioni moja.

Pia alisikika akimkosoa waziri mwenzake akisema hana akili,ana sura mbaya na anapenda sana kujigamba na kuwafokea watu.