Victor Moses

WASIFU WAKE: Victor Moses ni mchezaji mwenye umri wa miaka 22, ambaye kwa sasa anachezea klabu yake ya nne ya Liverpool huko England baada ya kuhama kwa mkopo kutoka klabu ya Chelsea jambo linalomweka kwenye mtihani wa kama ataweza kufurahia kiwango chake au atashindwa kudhihirisha kiwango chake.

Victor Moses ni raia wa Nigeria ambaye ana kila sifa ya kuchangia mafanikio makubwa kwenye timu. Ana kasi, ana uwezo wa kufunga magoli, ana uwezo wa kucheza nafasi tofauti uwanjani kutoka nafasi ya kiungo hadi ushambuliaji.

Moses alionja ladha ya kuchezea vilabu vikubwa katika ligi kuu ya England wakati alipojiunga na Crystal Palace klabu aliyoicheza klabu hiyo uanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2010 na kufanikiwa kufunga magoli 11 katika mechi 58 alizocheza kabla ya kuhamia klabu ya Wigan Athletic.

Katika miaka miwili akiwa Wigan, Victor Moses alifanikiwa kupachika wavuni magoli nane katika mechi 74 alizocheza.

Mwezi Agosti mwaka 2012, Moses alirudi tena London baada ya kununuliwa na Chelsea kutoka Wigan kwa uhamisho wa Paundi million 9.

Hata hivyo baadae Kocha Jose Mourinho ambaye alirudi kufundisha Chelsea kwa mara ya pili hakumweka Moses katika orodha ya wachezaji ambao ni chaguo lake.

Kwa sasa Moses amehamia Liverpool tangu mwezi Septemba mwaka huu kwa mkopo wa muda mrefu.

Akiwa Liverpool makali yake yameanza kuonekana ambapo katika mechi yake ya kwanza kwenye klabu hiyo alifunga bao pale timu hiyo ilipokutana na Swansea.

Moses ameshacheza mechi zaidi ya saba akiwa Liverpool na anaonekana kuwa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo walioifanya Liverpool ianze ligi kuu ya England kwa kishindo.

Kwa upande wa ngazi ya kimataifa Moses anachezea timu ya taifa ya Nigeria japokuwa alishawahi kuichezea England katika timu ya vijana hadi walio chini ya miaka 21.

Victor Moses ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria walioiwezesha kutwaa kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013.

Wadadisi wana maoni gani kumhusu Victor Moses?

Mwandishi wa BBC Nick Cavell anamwelezea Victor Moses ni mmoja wa wachezaji ambao wamekuwa hawapangwi kuanza kila mechi kwenye klabu yake au anapocheza timu ya taifa hii ni kwa lengo la kuongeza nguvu kwa wale wanaokuwa wanacheza.

Amekuwa akifurahia kila anapopewa nafasi uwanjani na hii imejidhihirisha kwa kazi yake anapokuwa uwanjani.

Pamoja na uwezo, uimara na shauku yake anapokuwa uwanjani Moses ni mshambuliaji ambaye anaweza kucheza nafasi yoyote na zaidi ya hayo amekuwa akifunga magoli muhimu na kwa wakati muhimu.

Mara chache amekuwa akitumiwa kama kiungo mchezeshaji lakini hufurahia zaidi anapochezeshwa kama mshumbuliaji ya nyuma.

Chelsea na Nigeria zinapaswa kumshukuru Moses kwa kuzisaidia timu zao kuchukua makombe muhimu mwaka 2013.

Kwa upande Chelsea Moses alifunga magoli muhimu siku ya roba fainali na nusu fainali ya ligi ya Europa ambapo baadae Chelsea ilinyakua kombe hilo.

Katika timu ya taifa ya Nigeria kwenye Fainali za kombe la Mataifa ya Afrika Victor Moses alikuwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu walioiwezesha kunyakua kombe hilo na alishiriki kupiga mikwaju ya penati muhimu za mwisho.

Umuhimu wake kwenye timu ya taifa unajidhirisha kwa kuteuliwa kwenye orodha ya wachezaji wanaounda kikosi cha timu hiyo japo amekosa mechi kadhaa za kufuzu kombe la dunia.

Kwa ujumla kwa mwaka mzima Moses amekuwa akikabiliwa na majeraha na kufanya akose baadhi ya mechi za kimataifa kwenye timu yake ya Nigeria.

Mbali na hayo kwa sasa Moses amejidhihirisha kuwa ni mmoja ya wachezaji muhimu katika kikosi cha Liverpool tangu alipojiunga na timu hiyo msimu huu wa ligi kuu ya England ambapo alifunga goli katika mechi ya kwanza wakati Liverpool ilipocheza na Swansea.

Akiwa pamoja na Luis Suarez na Daniel Sturridge ambao ni washambujiaji tegemeo wa Liverpool Moses amekuwa akipangwa ili kuwasaidia kama mshambuliaji anayewatengenezea nafasi.