Mpango wa chanjo watatizwa Sudan Kusini

Image caption Serikali na waasi wamezuia juhudi za kutoa chanjo ya polio kwa watoto Sudan Kusini

Juhudi za kuwapa chanjo ya ugonjwa wa kupooza watoto 165,000 zimetatizwa na mgogoro kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi, kwa mujibu wa mkuu wa misaada ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa.

John Ging amesema kuwa pande hizo mbili zinapaswa kukoma kutatiza shughuli hiyo na kuwaruhusu maafisa wa afya kuendelea na kazi yao ya kutoa chanjo katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

Maafisa wa Serikali pamoja na waasi wa SPLM-N walipuuza azimio la Umoja wa Mataifa lililowataka kuruhusu shughuli ya kutoa chanjo kuendelea.

Umoja wa Mataifa unahofia kuwa mgogoro katika majimbo hayo mawili, huenda ukasababisha mlipuko wa ugonjwa wa kupooza.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, ugonjwa wa Kupooza haujawahi kusikika SudanKusini angalau kwa zaidi ya miaka miwili.

Majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile inapakana na Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan na kujipa uhuru mwaka 2011 baada ya mazungumzo ya amani kumaliza vita vya muda mrefu.

''Umoja wa Mataifa ulifanya mazungumzo na serikali ya Sudan Kusini pamoja na vuguvugu la SPLM-N kuweza kuruhusu mpango wa kutolewa chanjo hiyo kuendelea kuanzia tarehe 5 Novemba hadi 12 Novemba lakini kwa bahati mbaya juhudi zetu zimekwamishwa,'' alisema bwana Ging baada ya kushauriana na baraza la usalama la UN.

Amesema kuwa UN inapaswa kutumia nguvu kulazimisha pande hizo mbili huruhusu mpango wa kutoa chanjo kuendelea.

Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Liu Jieyi, ambaye ni rais wa sasa wa baraza la usalama la UN, alisema hatua ya pande hizo mbili inaleta wasiwasi kuhusiana na mpango huo.

Hata hivyo hakuzungumzia hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya serikali na wapiganaji wa SPLM.

Alsema kuwa umoja wa mataifa tayari umekatiza mipango yake ya kutoa msaada wa chakula katika majimbo hayo na badala yake kuamua kuangazia mpango wake wa chanjo.

Takriban watu 800,000 waliathiriwa na mgogoro wa kisiasa ndani ya majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile na yamekosa msaada kwa miezi kumi na nane.

Punde tu baada ya Sudan Kusini kujitawala, mgogoro nao ukaanza kutokota katika majimbo hatyo mawili ya mpakani .