Meno ya Tembo yakamatwa Zanzibar

Image caption Meno ya Tembo yaliyokamatwa

Polisi nchini Tanzania wamekamata vipande elfu moja na ishirini na moja vya meno ya tembo vyenye uzito wa karibu kilo elfu tatu.

Meno hayo ya tembo yamekamatwa katika bandari ya Zanzibar jana na watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na meno hayo. Hata hivyo, bado haijafahamika idadi kamili ya tembo waliouawa, kwani baadhi ya meno yamekatwa vipande.

Kwa mujibu wa afisa habari mkuu wa jeshi la polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, kiasi kilichokamatwa ni kikubwa kuwahi kukamatwa visiwani humo.

Akizungumza na BBC jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema meno hayo yalikuwa yamehifadhiwa katika kontena la futi arobaini yakiwa yamechanganywa katika mifuko iliyohifadhi makombe ya konokono wa baharini, tayari kwa kusafirishwa nje.

Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.

Kukamatwa kwa meno haya ya tembo, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.

Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.

Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18 sawa na dola zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.