Wahamiaji 23,000 wa Ethiopia waondoka Saudia

Image caption Kuna takriban wahamiaji haramu milioni tisa nchini Saudi Arabia

Takriban raia 23,000 wa Ethiopia, wamejisalimisha kwa maafisa wakuu wa serikali ya Saudi Arabia tangu msako dhidi ya wahamiaji haramu kuanza nchini humo wiki jana.

Msako huo, umesababisha vurugu mjini Riyadh, watu watano wakipoteza maisha yao.

Maafisa wa utawala, wanasema kuwa wanajaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa asilimia 12 miongoni mwa wasaudia asilia.

Takriban wafanyakazi wahamiaji milioni tisa wanaishi nchini Saudi Arabia.

Wanasemekana kuwa nusu wa watu wanaofanya kazi nchini humo, hasa wakifanya kazi za makarani.

Balozi wa Ethiopia mjini Riyadh, Muhammed Hassan Kabiera, amesema kuwa ubalozi huo, umepata taarifa kuwa raia 23,000 wa Ethiopia tayari wamejikabidhi kwa maafisa wa utawala nchini humo.

Baadhi tayari wamerejeshwa nchini Ethiopia kikundi cha kwanza kikiwasili mjini Addis Ababa,mnamo siku ya Jumatano.

Katika makabiliano yaliozuka karibuni mjini Riyadh, raia mmoja wa Sudan aliuawa.

Wafanyakazi haramu walifanya vurugu na kuwarushia mawe madereva

Polisi hata hivyo waliweza kudhibiti hali.

Manfuhah ni mji unaokaliwa na idadi kubwa ya wahamiaji , wengi kutoka kanda ya Afrika Mashriki.

Mnamo siku ya Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom, alisema kuwa alikuwa na taarifa kuwa raia watatu wa Ethiopia waliuawa katika makabiliano yaliyozuka wiki jana.

Hata hivyo Maafisa wa Saudia walisema kuwa raia wawili wa kigeni pamoja na wenyeji watatu wa Saudia waliuawa kwenye vurugu hizo.

Mapema mwezi,huu maafisa walianza kuwakusanya wahamiaji haramu baada ya makataa ya miezi saba waliyopewa kupata stakabadhi halali za kuishi nchini humo kumalizika.

Karibia raia milioni moja wa Bangladesh, wahindi, wafilipino, raia wa Nepal, wapakistani na wayemeni, wanaaminika kuondoka nchini humo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.