Mazungumzo ya nyuklia:Iran haitayumba

Image caption Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa kidini Iran

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran ameionya nchi yake kutorudi nyuma hata kidogo kuhusu mpango wake wa nyuklia, wakati nchi hiyo ikiingia katika mazungumzo na mataifa sita makubwa duniani, kujadili mpango huo, mjini Geneva.

Ayatollah Ali Khamenei amesema hataingilia moja kwa moja mazungumzo hayo, lakini amewawekea mpaka katika mazungumzo hayo, wajumbe wa Iran.

Wakati huo huo Rais Barack Obama amewataka wabunge wa baraza la seneti la Marekani kutoiwekea Iran vikwazo zaidi ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa hatua za kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Amesema haijulikani kama itawezekana kufukia makubaliano hivi karibuni.

"Hatujui kama tutaweza kufikia makubaliano na Iran wiki hii au wiki ijayo," ameliambia jarida la Wall Street,(WSJ) mjini Washington,Jumanne.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa matumizi salama, lakini mataifa makubwa, yanashuku kuwa mpango huo wa Iran unalenga kutengeneza silaha za nyuklia.

Katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni Jumatano, Ayatollah Khamenei amesema wajumbe wa Iran katika mazungumzo ya Geneva, waliweka mpaka katika kujadili mpango huo kabla ya kusafiri kwenda Uswisi katika mkutano wa siku mbili na wawakilishi kutoka mataifa sita ambayo ni Marekani, Uingereza, Uchina na Urusi na Ujerumani.

Walishindwa kufikia mkataba katika awamu iliyopita ya mazungumzo mapema mwezi huu, kutokana na kile wanadiplomasia wanachosema msimamo wa Iran wa kutaka kutambuliwa haki yake ya kurutubisha madini ya urani, huku nayo Ufaransa ikihoji kuhusu mtambo wa nyuklia unaojengwa huko Arak.