Njia mpya ya Reli Afrika Mashariki

Image caption Njia hii ya reli itaunganisha Kenya na kanda nzima ya Afrika Mashariki na eneo la maziwa makuu

Kenya imezindua rasmi ujenzi wa njia ya Reli itakayounganisha kanda ya Afrika Mashariki na eneo la maziwa makuu ujenzi utakaofadhiliwa na serikali ya China.

Reli hiyo itaunganisha Kenya na Sudan Kusini, DR Congo na Burundi.

Sehemu ya kwanza ya njia hiyo ya reli , itaunganisha bandari ya Mombasa na Mji mkuu Nairobi na kupunguza muda wa safari kati ya miji hiyo kutoka masaa 15 hadi masaa manne tu.

Huu bila shaka ndio utakuwa mradi mkubwa Zaidi kuwahi kujengwa tangu nchi hiyo kujipatia uhuru miaka 50 iliyopita.

Mradi huo utagharimu dola bilioni 5.2 kiasi kikubwa cha pesa hizo kikitolewa na Uchina.

Baadhi ya wakenya wanalalamika kuwa tenda hiyo imetolewa kwa kampuni ya kichina kwa njia isiyofaa.

Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya uzinduzi huo amesema kuwa mradi huu ndio utakuwa kumbukumbu kubwa ya utawala wake Kenya.

Mkataba wa ujenzi wa njia hiyo ya reli, ulifikiwa kati ya Rais Kenyatta na mwenzake wa China Xi Jinping mnamo mwezi Agosti mjini Beijing.

Pia kuna matumaini kuwa njia hiyo ya reli itapunguza msongamano mjini Mombasa moja ya bandari yenye shughuli chungu nzima barani Afrika.

Njia ya reli iliyoko sasa, ni ile iliyojengwa enzi za ukoloni.

Baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza ya reli hiyo mjini Nairobi, mwaka 2017, itaendelezwa hadi Magharibi mwa DRC hususan mjini Kisangani, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

"Tunachokifanya hapa leo, kitaleta mageuzi makubwa sio nchini Kenya tu bali katika kanda nzima ya Afrika Mashariki,’’ alisema Rais Kenyatta akitaja mradi huo kama jambo la kihistoria.

Aliongeza kusema kuwa mradi huu ni moja ya miradi mikubwa katika maono yake ya maendeleo itimiapo mwaka 2030 kuboresha hali ya miundo msingi nchini humo.