Waandamanaji Thailand wavamia jeshi

Image caption Waandamanaji Thailand

Mamia ya waandamanaji nchini Thailand waliingia kwa nguvu katika makao makuu ya jeshi mjini Bangkok, ikiwa ni siku ya sita tangu kuanza kwa maandamano dhidi ya serikali.

Msemaji wa jeshi amesema waandamanaji walivunja kufuli la mlango mkuu na kuingia katika eneo la makao makuu hayo ya jeshi. Baadaye waliondoka.

Alhamisi, Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra aliwataka waandamanaji kuacha maandamano mitaani, ikiwa ni baada ya waziri mkuu huyo kushinda kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa bungeni.

Lakini kiongozi wa waandamanaji Suthep Thaugsuban amekataa ombi hilo.

"Hatutaacha waendelee na kazi," mbunge mwandamizi wa zamani wa upinzani alisema hayo katika hotuba yake, Alhamisi.

Waandamanaji wapatao 1,000 waliingia kwa nguvu katika viwanja vya makao makuu ya jeshi mjini Bangkok.

Msemaji wa jeshi Kanali Sansern Kaewkamnerd amesema waandamanaji hawakuingia katika majengo.

Mwandishi wa BBC, Jonah Fisher, ambaye yupo katika eneo la tukio, amesema waandamanaji walikusanyika nje ya jengo wakisikiliza hotuba za viongozi wao waliokuwa katika jukwaa walilojenga.

Walikuwa wakiomba jeshi liwaunge mkono waandamanaji. "Tunataka kujua jeshi liko upande gani," Shirika la Habari la Uingereza, Reuters lilimkariri mmoja wa waandamanaji akisema hivyo.

Serikali imewataka waandamanaji kufanya mazungumzo-lakini ombi hilo limekataliwa.

Mwandishi wetu ameelezea hali hiyo kuwa nzuri na kusema serikali inaonekana kuepuka malumbano.