Mgogoro wa Ukraine:Mazungumzo kuanza

Image caption Maelfu ya waandamanaji mjini Kiev, Ukraine

Mazungumzo kati ya serikali ya Ukraine na viongozi wa upinzani yanatarajiwa kuanza leo,Jumatatu kufuatia maandamanao ya siku kadha katika mji mkuu Kiev.

Spika wa bunge la Ukraine, Vlodymyr Rybak ameahidi kuwa pande zote zinazohusika na mgogoro huu zitapata nafasi ya kutoa maoni yao.

Waandamanaji waliingia katika mitaa wakipinga uamuzi wa Rais Viktor Yanukovych kukataa kutia saini mkataba ambao ungeiweka Ukraine karibu zaidi na Umoja wa Ulaya. Kutokana na hatua hiyo ya Rais Yanukovych, waandamanaji wamemtaka kujiuzulu.

Baadhi ya viongozi wao wamesema watajaribu na kulazimisha serikali kujiuzulu na watashawishi kugomewa kwa mkutano wa baraza la mawaziri. Mapigano makali kati ya wanaharakati na majeshi ya usalama yaliendelea Jumapili katika mji mkuu Kiev.

Bwana Yanukovich anasema badala ya kushirikiana na Umoja wa Ulaya, anataka kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Urusi.

Mapema Jumatatu, mamia ya wanaharakati walikuwa wameendelea kuzingira ukumbi wa mikutano wa jiji, mjini Kiev.

Maelfu zaidi wamekesha katika medani ya Independence.