Waziri wa Nigeria ashinda tuzo ya Forbes

Image caption Akinwumi Adesina, waziri wa kilimo Nigeria

Waziri wa Kilimo wa Nigeria Akinwumi Adesina ametangazwa na jarida la Forbes Afrika kuwa mshindi wa mwaka kutokana na mageuzi yake katika sekta ya kilimo.

"Ni mtu ambaye yuko katika mwelekeo wa kuisaidia Afrika kujilisha," amesema mhariri wa Forbes Africa,Chris Bishop.

Wachambuzi wa mambo wanasema uchumi wa Nigeria kwa muda mrefu ulihodhiwa na mafuta ya petroli, wakati kilimo kikipuuzwa, japokuwa kilimo kinategemewa na watu wengi.

Bwana Adesina amesema anataka kuwasaidia watu kutajirika kupitia kilimo.

"Lengo langu ni kuwafanya watu wengi mamilionea, hata kuwa mabilionea, kutoka sekta ya kilimo haraka iwezekanavyo," amesema katika hotuba ya kukubali tuzo hiyo.

Aliyu Tanko kutoka Idhaa ya Hausa ya BBC, amesema Adesina ameanzisha uwazi zaidi katika usambazaji na ugawaji wa mbolea, shughuli ambayo katika siku za nyuma iligubikwa na rushwa kubwa.

Wanaigeria wengi wanaishi katika dimbwi la umaskini, hususan katika maeneo ya vijijini.

Waziri pia amewataka raia wa Nigeria kulima zaidi mazao ya chakula, hasa zao la mhogo.

Mwezi Januari, Bwana Adesina alitangaza mpango wa kuwagawia simu za mkononi wakulima milioni kumi "ili kuleta mageuzi ya kilimo nchini humo," kwa hiyo wanaweza kupata taarifa mpya za masoko.

Simu hizo pia zinatumika kupata vocha za mbegu na mbolea.

Hata hivyo mwandishi wetuamesema lengo hili bado halijafikiwa, akibainisha kuwa hakuna mtandao mzuri wa simu katika maeneo mengi ya vijijini nchini humo.

Chama kikuu cha upinzani kilikosoa mpango huo kuwa ni "zoezi la kutafuta kura".

Bwana Adesina aliwashinda baadhi ya wafanyabiashara wakubwa barani Afrika: Aliko Dangote na Jim Ovia, pia kutoka Nigeria; Patrice Motsepe kutoka Afrika Kusini na Strive Masiyiwa wa Zimbabwe.

Japokuwa nchi yao ni moja ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani, wengi wa raia wa Nigeria wanaishi katika hali ya umaskini mkubwa, hususan katika maeneo ya vijijini.

Bwana Bishop amesema ana matumaini kuwa tuzo hiyo itawahamasisha watu wengi barani Afrika kupanda mazao ya chakula chao wenyewe.