Makasisi watakaowanajisi watoto watakiona

Image caption Papa Francis kupambana na makasisi wanaowaharibu watoto

Baba mtakatifu Papa Francis ameidhinisha kamati ya Vatican itakayopambana na visa vya unajisi wa watoto katika kanisa katoliki pamoja na kuwasaidia waathiriwa kwa kuwapa ushauri nasaha.

Tangazo hili limelotolewa na naibu askofu mkuu Sean O'Malley mjini Boston Marekani, na linakuja baada ya kufanyika mkutano kati ya Papa na makadinali wake wanane ambao humshauri.

Kadhalika tangazo lenyewe linakuja baada ya Vatican kukataa ombi la Umoja wa Mataifa la kutaka ukabidhiwe taarifa za kanisa hilo kuhusu madai ya makasisi na watawa wanaodaiwa kuwanajisi watoto.

Papa Francis, amesema kuwa swala la kukabiliana na visa vya makasisi kuwanajisi watoto ni muhimu sana ili kuweza kulirejeshea hadhi kanisa Katoliki.

Kadinali, Sean O'Malley, naibu askofu mkuu wa kanisa hilo mjini Boston, alisema kuwa kamati hiyo inaweza kutoa mwongozo wa kikazi kwa makadinali na maafisa wa kanisa ili kulainisha utenda kazi wa viongozi wa kanisa.

Mji wa Boston ndio ulikuwa kitovu cha madai ya makasisi kuwanajisi watoto nchini Marekani mwaka 2002.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, naibu Askofu alisema kuwa kamati hiyo mpya ilipendekezwa na baraza la makadinali, ambalo lilibuniwa ili kufanyia mageuzi kanisa katoliki. Papa aliliidhinisha Alhamisi.