Wizara ya ulinzi yashambuliwa Yemen

Image caption Shambulio katika wizara ya ulinzi, Yemen

Bomu lililokuwa limetegwa katika gari limelipuka katika wizara ya ulinzi katika mji mkuu Sanaa nchini Yemen na kuua watu wapatao 20 na kujeruhi wengi.

Moshi ulionekana kutoka katika jengo la eneo la kibashara la Bab al-Yaman, katika lango la kuingilia katika mji mkongwe.

Kulikuwa na taarifa za mapigano ya bunduki ndani ya eneo hilo, lakini maafisa wanasema hali ilikuwa imedhibitiwa.

Majeshi ya usalama ya Yemen yanapambana na waasi kutoka eneo hilo na kikundi cha al-Qaeda, huku wakikabiliana na ukiukwaji wa sheria na mgawanyiko wa jeshi.

"Shambulio hilo limefanyika muda mfupi baada ya saa za kazi kuanza katika wizara hiyo, wakati dereva wa gari lenye bomu alipoendesha gari hilo kuingia ndani ya wizara ya ulinzi," taarifa ya wizara imesema, ikikaririwa na shirika la habari la Uingereza, Reuters.

Mlipuko huo ulisikika katika umbali mrefu kutoka eneo la tukio.

"Mlipuko huo ulikuwa unatisha sana, eneo lote lilitikisika kwa sababu ya mtikisiko huo, huku moshi ukionekana kutoka jengo hilo," shuhuda mmoja ameliambia shirika hilo.

Maafisa wamesama gari la pili lilifuata ambapo watu waliokuwa ndani ya gari hilo walifyatua risasi katika jengo hilo, na mapigano hayo yakiwahusisha watu wenye silaha wakiwa wamevalia sare za jeshi.

Eneo hilo limezuiliwa na watu waliouawa wamepelekwa katika hospitali ya jeshi iliyopo katika eneo hilo.

Taarifa zisizothibitishwa zinasema kuwa hospitali yenyewe ililengwa na wapiganaji, lakini maafisa wamesema hali hiyo kwa sasa inadhibitiwa.

Tukio hili limefanyika huku kukiwa na ulinzi mkali katika wiki chache zilizopita kufuatia mfululizo wa mashambulio ya kushtukiza dhidi ya maafisa wa serikali yanayoendeshwa na wapiganaji ambao hutumia pikipiki, wakihusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda wanaoendesha shughuli zao katika rasi ya Uarabuni, AQAP.

Yemen imekuwa katika matatizo makubwa tangu Rais Ali Abdullah Saleh aondolewe madarakani mwaka 2011.