Maandamano yakithiri Bangkok,Thailand

Image caption Maandamano yamesababisha serikali kuitisha uchaguzi mpya

Maelfu ya waandamanaji wanaopinga serikali wamefurika katika barabara za mji mkuu wa Thailand ,Bangkok licha ya serikali kutangaza uchaguzi wa mapema nchini humo.

Waziri mkuu Yingluck Shinawatra alitoa taarifa katika Runinga kabla ya maandamano hayo kuanza na kusema kuwa analivunja bunge ili kuitisha uchaguzi mpya nchini humo hivi karibuni.

Kiongozi wa maandamano hayo Suthep Thauksuban amesema kuwa ataendelea na vita hivyo na akawaambia waandamanaji kuwa wameshinda vita vikubwa dhidi ya serikali.

Kiongozi huyo alikuwa amekataa kufanyika kwa uchaguzi mpya na badala yake anataka kubadilishwa kwa serikali hiyo na kile alichokitaja kama baraza la raia.

Wabunge wote wa chama cha upinzani cha Demokrat walijiuzulu bungeni hapo jana.