Polisi 5 wauawa mpakani mwa Kenya na Somalia

Image caption Al Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia katika mpaka wa Kenya na Somalia

Idara ya polisi nchini Kenya imesema kuwa polisi watano na raia wawili wameuawa katika shambuliai dhidi yao kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.

Polisi wengine wawili hawajulikani waliko.

Shambulizi hilo lilifanyika katika barabara iliyoko kati ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Dadaab na mji wa Mashariki wa Liboi.

Polisi hao waliuawa wakiwa wanashika doria wakati gari lao liliposhambuliwa kwa risasi.

Mpaka wa Kenya na Somalia umekuwa kitovu cha mashambulizi ya kuvizia yanayofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabaab pamoja na makundi mengine ya watu waliojihami.

Mashambulizi ya mara kwa mara hufanyika kwenye mpaka huo ingawa haijulikani nani aliyehusika na shambulizi la leo.

Wanamgambo wa Al-Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi Kenya na la hivi karibuni likiwa lile lililofanywa dhidi ya jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi ambapo waliwateka watu nyara na kuwaua wengine mwezi Septemba.

Watu 61 waliuawa na wengine miambili kujeruhiwa vibaya.