Maelfu wamuaga shujaa wa Afrika Mandela

Image caption Katibu mkuu wa UN, Ban Ki Moon , Rais Barack Obama na Jacob Zuma

Zaidi ya maraisa tisini wameungana na wananchi wa Afrika Kusini katika misa ya wafu ya Nelson Mandela na kusimulia kumbukumbu zao kwa Shujaa huyo wa Afrika.

Akiongea kwenye mkusanyiko huo mjini Soweto, Rais wa Marekani Barack Obama alimtaja Mandela kuwa shujaa na mkombozi wa Afrika na shujaa shupavu kuwahi kuonekana katika karne ya ishirini.

Alisema maisha ya Mandela lazima yawe mfano mzuri kwa dunia nzima hasa vita alivyopigania kuhakikisha utu wa watu unaheshimiwa.

Jamaa za Mandela wamemtaja baba yao Mandela kama mtu aliyetaka watu kuwa sawa.

Mmoja wa wajukuu wa Mandela alikariri shahiri la kusisitiza mshikimano wa watu. Obama alishangiliwa ingawa Rais Jacob Zuma anayehutubia wananchi alizomewa mara kwa mara.

Uwanja ambako misa hiyo inafanyika, haukujaa watu kutokana na mvbua kubwa iliyonyesha.

Maelfu ya watu wamehudhuria misa hiyo katika uwanja wa FNB.

Afrika Kusini imeandaa shughuli mbali mbali za kumuenzi Mandela kabla ya siku ya kuzikwa kwake nchini Afrika Kusini siku ya Jumapili.

Misa ya leo ni moja ya mikusanyiko mikubwa ya viongozi wa kimataifa iliyoshuhudiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Viongozi wengine Watakaohudhuria misa ya wafu ya Mandela:

Watu wengi walikaidi hali mbaya ya hewa ambapo mvua kubwa imenyesha huku wakikusanyika uwanjani humo wakisubiri kwa muda mrefu kabla ya misa hiyo kuanza muda mfupi uliopita.

Waliohudhuria misa hiyo wamesemekana kuwa wenye furaha wakiimba nyimbo na kutaja jina la Mandela kwa shangwe unaweza kudhani ni mkutano wa kisiasa.

Misa hiyo itafanyika katika uwanja ambako Nelson Mandela alionekana kwa mara ya mwisho hadharani.

Misa hiyo itaonyeshwa kwenye skrini kubwa nje ya uwanja ili kuzuia msongamano wa watu.

Mandela alifariki akiwa na umri wa miaka 95 na kwa wengi yeye ni shujaa na mkombozi wa Afrika Kusini.