Maadhimishyo ya miaka 50 - Kenya

Image caption Kenya at 50

Maelfu ya watu wamekusanyika katika Uwanja wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi kuadhimisha miaka 50 tangu nchi hiyo ijipatie uhuru wake. Takriban marais 15 kutoka nchi mbali mbali za Afrika na waakilishi wa marais wakiwemo manaibu wao na mabalozi na wageni wengine wa heshima wamefika kutoa pongezi zao kwa nchi hiyo.

Miaka 50 iliyopita Kenya ilikata minyororo ya ukoloni kutoka kwa Uingereza.

Licha ya misuko suko, na mitihani iliyokumba nchi hiyo wananchi wameelezea kufurahia hatua walizopiga katika nyanja mbali mbali tangu kushikilia usukani wa nchi yao wenyewe.

Mbwembwe na densi ndio picha kutoka uwanja wa Kasarani tangu alfajiri watu walipoanza kukusanyika kwa sherehe hizo. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alianzisha rasmi sherehe saa sita usiku wa kuamkia Alhamisi, kwa kuipandisha bendera ya nchi kama ishara na kumbu kumbu ya mambo yalivyokuwa miaka 50 iliyopita wakati nchi hiyo ilipopandisha bendera hiyo kwa mara ya kwanza.

Tangu kupandishwa bendera hiyo sherehe hazijasimama na zimepangiwa kufanyika kwa siku nyingi. Rais Kenyatta ametoa siku 3 za likizo kuwapa wananchi fursa ya kusherehekea.

Viongozi wahutubia

Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewapongeza wananchi wenzake na kuwahimiza wawe naumoja na wakomeshe ufisadi. Lakini rais Kenyatta pia alikuwa na ujumbe wa mataifa ya magharibi.

''Ninao ujumbe kwa hao marafiki zetu. Ni muhimu sana kwao kutambua kuwa Afrika imehitimu. Afrika inataka kupewa ushirikiano utakaoifaidi. Tutakubali tu washirika wanaotuheshima namna tunavyowaheshimu. ni ushindi wa pande zote. Hatutakubali ushirikiano ambao hautambuwi kuwa pia sisi tunao uwezo wa kuchangia maamuzi, na kuwa tunayo sauti. Afrika inayo sauti. na miaka 50 baada ya kujitawala, sasa Afrika inataka sauti yake pia isikike.''

Museveni

Miongoni mwa wageni wa heshima waliohutubia umati wakati wa sherehe hizo ni rais wa nchi jirani, Uganda, Yoweri Kaguta Museveni. Alikuwa na ujumbe mkali kwa wababe aliodai kuwa bado wana nia ya kuzitawala nchi za Afrika.

''Nataka kutoa pongezi zangu kwa Wakenya, kwa kukataa ubabe wa wakoloni mwaka huu. Ni katika njia mliopiga kura. Cheers......! licha ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wakiwataka mpige kura wapendavyo wao, nyinyi Wakenya mlikataa kuwasikiliza. Hongera!. Hiyo ni sawa na kuikomboa Kenya mara ya pili baada ya ukombozi wa Mau Mau. Kama Muungano wa Afrika, tumewaandikia kuwaambia waachana na Mambo ya Kenya. Watu wengine wanatuambia haituhusu..... Mimi nimehusika katika kupigania ukombozi miaka mingi na nawasihi Wakenya, msiwe na hofu. Kama hawana macho basi tutawaonesha.''