Jaji:Udukuzi unakiuka katiba Marekani

Image caption Marekani imepuuza pendekezo la kumsamehe Edrward Snowden ili akome kufichua taarifa zaidi

Jaji wa mahakama katika jimbo moja nchini Marekani amesema kuwa mtindo wa shirika la ujasusi la Marekani kukusanya data za kwenye simu za watu binafsi ni kinyume na katiba ya nchi.

Jaji Richard Leon alisema kuwa tabia hiyo inaingilia taarifa za faragha za watu na kuwa haistahili na pia wamarekani hawaishi kwa amani kwani simu zao zote zinadukuliwa.

Mmoja wa watu waliolishitaki shirika hilo kwa kufanya udukuzi wa simu za mkononi za watu na kukusanya data nyingi ya watu binfasi Lary Klayman, amesema kuwa shirika hilo sharti lijue kuwa linakwenda kinyume na sheria.

Larry Klayman aliongea na BBC baada ya jaji Richard Leon, kuamua udukuzi wa simu unaofanywa na shirika la ujasusi la Marekani unakiuka katiba ya nchi kuhusiana na kukusanya taarifa kwa njia isiyofaa.

Baadhi ya taarifa ambazo hukusanywa na shirika hilo ni namba za simu za watu, nyakati walizopiga simu na tarehe walizopiga simu zao.

Sakata hili lilifichuliwa na mtoro Edward Snowdon kuhusu tabia ya serikali ya Marekani kufanyia simu za watu udukuzi katika juhudi zao za kutafuta taarifa za kijasusi.

Jaji Leon alitoa agizo la muda la kuzuia shirika hilo kuendeleza udukuzi ingawa anasuburi serikali kukata rufaa.

Ikulu ya White House ilipuuzilia mbali pendelezo kuwa Bwana Snowden ambaye alikimbilia nchini Urusi baada ya kufichua taarifa hizo kupewa msamaha ili aweze kukoma kuendelea kufichua taarifa hizo.