Askofu Desmond Tutu akemea ANC

Image caption Askofu Tutu ametishia kutokipigia tena kura chama cha ANC

Askofu mkuu nchini Afrika Kusini Desmond Tutu, amesema kuwa Nelson Mandela angechukizwa sana na ANC kukosa kuwajumuisha watu wa jamii ya Afrikaners kwenye ibada za mazishi yake.

Alichokikosoa zaidi ni kutoshirikisha kanisa la (Dutch Reformed Church) na kukosa kutumia pakubwa lugha ya Afrikaans kwenye ibada hizo.

Chama rasmi cha Afrikaan ndicho kilichoanzisha utawala wa kizungu nchini Afrika Kusini, utawala ambao Mandela alipinga na hata kufungwa jela miaka 27.

Lakini baada ya kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mandela alihutubu zaidi kuhusu maridhiano na msamaha kwa maadui.

Tutu alikosoa vikali ambavyo chama tawala cha ANC kiliendesha hafla za kumuenzi Mandela alipofariki hadi alipozikwa.

"Ninaamini kuwa ujumbe ambao ungetolewa ikiwa viongozi wa ANC wasingesimamia hata hafla ya mazishi, ungekuwa wa maridhiano.''

Tutu alipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi akishirikiana na Mandela pamoja na chama cha ANC, lakini katika siku za hivi karibuni amekuwa akikosoa sana chama cha ANC na hata kutishia kuwa atapigia kura upinzani.

Nusura akose kuhudhuria mazishi ya Mandela akisema kuwa hakualikwa.

Katika taarifa yake alimtaja Mandela kama mjenzi wa taifa na mtu aliyejitolea kuwajumuisha waafrikaans kwenye uongozi wake baada ya enzi ya ubaguzi wa rangi.

" Sote tumekosa sana kwa kutokuwa watu wa kuwajumuisha wengine kama alivyokuwa Madiba,'' alisema Tutu.

"kwa hivyo mimi nawaomba msahama ndugu zetu wa jamii ya Afrikaans,'' aliongeza Tutu.