Mali: chama cha rais Keita chashinda

Kwa mujibu wa matokeo ya awali nchini Mali ,Muungano wa vyama mbalimbali vinavyomuunga mkono Rais wa Mali, Ibrahim Boubakar Keita vimeshinda uchaguzi wa bunge.

Chama cha RPM na washirika wake wamejinyakulia viti 115 kati ya 147 katika Bunge la taifa hilo baada ya duru la pili la uchaguzi lililofanyika mwishoni mwa juma lililopita. Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura kwa awamu zote imeelezwa kuwa chini.

Uchaguzi huu umeelezwa kuashiria kurejea kwa demokrasia baada ya mapinduzi ya mwaka 2012.

Ufaransa bado ina Wanajeshi wake takriban 3000 nchini humo baaa ya kuingia mwezi Januari kwa ajili ya Operesheni ya kuyaondoa makundi ya kiislamu ambayo yalikuwa yakidhibiti eneo la kaskazini mwa Mali.

Mali ilifanya uchaguzi wa amani kuchagua Rais mwezi Agosti, lakini tangu wakati huo kumekuwepo na hali ya ukosefu wa usalama.

Matokeo ya uchaguzi wa bunge, yatakuwa rasmi mara baada ya mahakama ya kikatiba itapotoa matokeo yake baadae juma hili.

Maafisa walisema kuwa chama cha Union for the Republic and Democracy (URD) kilipata viti kati ya 17 na 19, matokeo yanayomfanya mgombea wa zamani wa uchaguzi wa Urais Soumaila Cisse kuwa Kiongozi wa upinzani.

Idadi ya waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 37.2% tofauti na ile ya 38.6% katika duru ya kwanza ya uchaguzi hali inayoelezwa kutoridhisha.

Vikosi vya kijeshi MINUSMA pia vimepeleka wanajeshi zaidi ya 6,000 na Polisi, ingawa kumekuwa na mafanikio katika hilo, bado makundi ya kiislamu yamekuwa kikwazo kwao.